2017-06-30 16:44:00

Makatibu wakuu wa CCEE wanapembua changamoto za Kanisa Barani Ulaya


Makatibu wakuu kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, kuanzia tarehe 30 Juni hadi tarehe 3 Julai 2017 wanafanya mkutano wao wa 45 unaotafakari pamoja na mambo mengine, dhamana na mchango wa Kanisa katika Jamii mchanganyiko, mintarafu masuala ya kijamii, kitamaduni na kiuchumi. Mkutano huu unaofanyika huko Bucharest, nchini Romania unapembua kwa dhati kabisa mchango wa Kanisa Barani Ulaya, kwa kutambua changamoto zilizopo na hatimaye, kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yake katika medani mbali mbali za maisha!

Mkutano huu unawashirikisha viongozi wakuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya na pamoja na uwepo wa Askofu mkuu Miguel Maury Buendìa, Balozi wa Vatican nchini Romania na Moldova. Uwepo wa Kanisa Katoliki nchini Romania katika kipindi cha Miaka 10 ni kati ya mada ambazo imefanyiwa kazi wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Makatibu wakuu wa Shirikisho hili. Ni nafasi ya kusali, kutafakari na kushirikisha uzoefu na mang’amuzi ya maisha na utume wa Kanisa katika medani mbali mbali.

Wajumbe pia wanachambua masuala ya tunu msingi za maisha ya kifamilia, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa ni changamoto kubwa kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni nafasi pia ya kuanza maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu vijana itakayofanyika mjini Vatican, Mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”. Ulinzi na usalama kwa watoto dhidi ya nyanyaso za jinsia, majadiliano ya kidini na kiekumene ni mambo ambayo pia yamo kwenye ajenda za mkutano huu. Wakati wa mkutano huu, Makatibu wakuu watapata nafasi ya kutembelea nyumba kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, Kanisa linalojengwa huko Kusini mwa Mji wa Bucharest pamoja na mahali alipozaliwa Mfiadini Vladimir Ghika pamoja na mashuhuda wengine wa imani. Makatibu wakuu watasikiliza pia taarifa mbali mbali kutoka kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya na Jumatatu, tarehe 3 Julai, 2017, wajumbe watafanya mkutano wa faragha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.