2017-06-30 16:32:00

Familia ya Mungu Sudan ya Kusini inamshukuru Papa Francisko!


Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan, SCBC, linamshukuru sana Baba Mtakatifu Francisko kwa kuonesha moyo wa upendo na ukarimu wa Kibaba kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, ambayo kwa sasa imeelemewa na vita ya wenyewe kwa wenyewe, njaa na ukame wa kutisha. Shukrani hizi zimetolewa na Askofu Edward Hiiboro Kussala, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan. Hivi karibuni, Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu alitangaza kwamba, kwa sasa hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko iliyokuwa ifanyike mwezi Oktoba, 2017 imeahirishwa hadi wakati mwingine tena, lakini Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini inayokabiliwa na changamoto nyingi kwa wakati huu.

Baba Mtakatifu akaamua kuchangia kwa hali na mali mradi ambao unajulikana kama “Baba Mtakatifu kwa ajili ya Sudan ya Kusini”. Huu ni mradi unaopania kusaidia shughuli mbali mbali za huduma na maendeleo zinazotekelezwa na Mashirika ya kitawa na kazi za kitume pamoja na Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa ya Misaada huko nchini Sudan ya Kusini. Haya ni mashirika ambayo licha ya vita na ghasia kuendelea kupamba moto nchini Sudan ya Kusini, lakini yamekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu. Kwa njia hii, amani ya kweli na dumifu inaweza kupatikana hata Sudan ya Kusini.

Askofu Edward Hiiboro Kussala anapenda kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuonesha upendo na mshikamano wa dhati kwa njia ya ushuhuda wa mchango wake wa dola za kimarekani 500, 000 ambazo zitatumika kama zilivyokusudiwa na Baba Mtakatifu na kwamba, wanamshukuru kwa kuendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka zake. Ni matumaini ya familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini kwamba, iko siku Baba Mtakatifu ataweza kuitembelea na kwamba, iko siku haki, amani, upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa vitaweza kushamiri katika akili na nyoyo za watu, kumbe, hakuna sababu ya kukata tamaa.

Sudan ya Kusini, tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Sudan Kongwe, imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi hasa kutokana na madhara ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo ilisababisha watu wengi kupoteza maisha yao na wengine wengi walijikuta wakiwa wanaishi kama wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi ya kudumu. Tangu mwanzo, kumekuwepo na hali tete ya kisiasa nchini humo kutokana na uchu wa mali na madaraka. Kanisa katika hali, mazingira na changamoto hizi anasema Askofu Edward Hiiboro Kussala bado linaendelea kusimama kidete kutangaza na kushuhudia ukuu na utakatifu wa maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan linapenda kusimama kidete kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Sudan ya Kusini. Kanisa linapenda kuonesha upendo na mshikamano kwa njia ya huduma kwa waathirika wa majanga asilia, vita, ghasia na kinzani za kijamii. Ni matumaini ya familia ya Mungu kwamba, iko siku Baba Mtakatifu Francisko ataitembelea ili kuitangazia Injili ya amani, upendo na mshikamano wa dhati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.