2017-06-29 15:27:00

Mitume Petro na Paulo ni mashuhuda wa imani walioyamimina maisha yao!


Maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani ni ushuhuda wa maisha ya mitume walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kiasi kwamba, wamekuwa ni mashahidi wa Kristo katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, hata miisho ya dunia. Mitume walisimama kidete: kukiri, kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Walimkiri na kutamka wazi wazi kwa kinywa cha Mtakatifu Petro kwamba, Yesu kwa hakika ni Mwana wa Mungu aliye hai.

Licha ya udhaifu na mapunguzu ya Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake, lakini Kristo aliamua kumpatia ukuu na mamlaka akisema, “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni: na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni! (Rej. Mt. 16:18). Mtakatifu Paulo, mtume na mwalimu wa mataifa anakaza kusema Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, akawa kwake ni sababu ya habari za nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa.

Daima, Mababa wa Kanisa wamesikika wakisema, damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo sehemu mbali mbali za dunia, changamoto ni kukuza na kudumisha uekumene wa damu unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Mashuhuda wa imani ni kielelezo makini cha mateso na kifo cha Kristo Msalabani! Kumbe, maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani ni kielelezo cha furaha ya ufufuko wa wafu na ushindi dhidi ya dhambi na mauti; ni fursa ya kumtafakari Kristo anayeketi kuume kwa Baba yake wa mbinguni!

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, aliomwandikia Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani; watu ambao kwa njia ya maisha na mafundisho yao, wameweza kumtangaza na kumshuhudia Kristo kati ya watu wa Mataifa. Leo hii Kanisa linahamasishwa kuwa ni shuhuda wa mateso, dhuluma na nyanyaso sehemu mbali mbali za dunia. Inasikitisha kuona kwamba, Wakristo wanafukuzwa hata katika maeneo yao ya asili, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kujenga umoja na mshikamano kama sehemu ya uekumene wa damu.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakaza kusema, Makanisa hayana budi kushikamana katika uekumene wa sala, kwa ajili ya kuombea: haki, amani, umoja na mshikamano, kama walivyofanya wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri hivi karibuni. Makanisa hayana budi kushirikiana dhidi ya vitendo vya kigaidi na uvunjifu wa haki msingi za binadamu ili kuheshimu, utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu. Wakristo waendelee kushikamana na kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema katika kupigania haki na amani duniani; kwa kushuhudia: ukweli na uwazi; uaminifu, huruma, upendo na mshikamano wa dhati! Majadiliano ya kidini na waamini mbali mbali duniani hayana budi kuendelezwa na wote, ili kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza.

Majadiliano haya yanaweza kuwa na tija, ikiwa kama yatatekelezwa na Wakristo walioungana na kushibana; waamini wanaoweza kusimama kidete kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo na kwa njia hii, wote watawatambua kuwa kweli wamekuwa ni wafuasi amini wa Kristo Yesu! Majadiliano ya kiekumene yajengeke katika msingi wa ukweli na upendo; mshikamano na ushirikiano wa kidugu kama ilivyojitokeza katika mkutano wa kumi na nne wa Tume ya Pamoja ya Majadiliano ya Kitaalimungu Kimataifa huko Chieti pamoja na kuendelea kukazia umuhimu wa sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Mwishoni, Patriaki Bartolomeo wa kwanza, anamwombea Baba Mtakatifu Francisko afya njema, amani na utulivu, ili aweze kuendeleza huduma kwa familia ya Mungu aliyokabidhiwa kwake na Kristo Yesu! Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza uliwasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 27 Juni 2017 na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza ulioongozwa na Askofu mkuu Job wa Telmessos, Mwenyekiti mwenza wa Tume ya Pamoja ya Majadiliano ya Kitaalimungu Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.