Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Makardinali wapya kumbatieni Msalaba wa Kristo!

Papa Francisko, Jumatano tarehe 28 Juni 2017 amewasimika Makardinali wapya 5 ambao sasa wanakuwa ni sehemu ya Baraza la Makardinali, mwashauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. - AFP

29/06/2017 07:00

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano jioni, tarehe 28 Juni 2017 ameongoza Ibada ya kuwasimika Makardinali wapya watano ambao kwa sasa wanakuwa ni sehemu ya Baraza la Makardinali ambalo lina jukumu la kumshauri Khalifa wa Matakatifu Petro mintarafu maisha na utume wa Kanisa la Kristo! Makardinali wapya ni kama wafuatavyo:

Kardinali Jean Zerbo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bamako, Mali.

Kardinali Juan Jose Omella, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Barcelona, Hispania.

Kardinali Anders Arborelius, Askofu wa Jimbo Katoliki la Stockholm, Sweden.

Kardinali Louis-Marie Ling Mangkhanekhoun, Askofu wa Laos, Cambodia.

Kardinali Gregorio Rosa Chàvez, Askofu msaidizi Jimbo kuu San Salvador, El Salvador.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amewakumbusha Makardinali wapya kwamba, daima Yesu atatangulizana nao katika maisha na utume wao, kama alivyofanya kwa Mitume wake alipokuwa anatangaza mara ya tatu kuhusu kuteswa na kufufuka kwake. Yesu aliwajulisha mitume wake kuhusu mateso yaliyokuwa mbele yake, lakini kulikuwepo na pengo kubwa kati ya kile kilichokuwa kimehifadhiwa moyoni mwa Yes una kile ambacho kilikuwa kimehifadhiwa katika sakafu ya mioyo ya mitume wake. Pengo hili lingeweza kuzibwa na Roho Mtakatifu peke yake. Kutokana na hali kama hii, Yesu alionesha uvumilivu mkuu, akazungumza na mitume wake katika ukweli na uwazi, lakini zaidi, akawatangulia na kutembea mbele yao!

Baba Mtakatifu akaza kusema, mitume wakiwa njiani, walijikuta wanapoteza mwelekeo, kinyume kabisa cha Yesu aliyekuwa anapania kutimiza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni! Wao wakaanza kugombania madaraka na nafasi za upendeleo kama ilivyotokea kwa Yakobo na Yohane wana wa Zebedayo. Walidhani kwamba, wamefahamu, lakini kumbe, walikuwa wamezama katika ombwe; walidhani kwamba, walikuwa wanaona, kumbe, walikuwa wanatembea katika giza nene! Walidhani kwamba, wao walikuwa na ufahamu mkubwa kuliko wengine, kumbe, walikuwa si mali kitu!

Baba Mtakatifu anasema, ukweli ambao Kristo Yesu alipenda kuwafunulia mitume wake ni juu la Fumbo la Msalaba na uwepo wa dhambi duniani, kazi ambayo amekuja kuifanya humu ulimwenguni ni kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mwaliko kwa wafuasi wa Kristo ni kushiriki katika kazi hii ya kuwakomboa watu wanaoogelea na kupoteza maisha kutokana na: vita, ghasia; vitendo ya kigaidi; mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo inayonyanyasa utu na heshima ya binadamu hata wakati huu ambapo haki msingi za binadamu zinaendelea kupigiwa debe sana!

Ni mwaliko wa kuangalia kambi za wakimbizi na wahamiaji ambazo zimegeuka kuwa ni mazingara hatari sana kwa utu, heshima na maisha ya binadamu. Kuna utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, utu na heshima ya binadamu vinapimwa kutokana huduma anayoweza kutoa mtu, kinyume cha hapo si mali kitu! Haya ndiyo ambayo Yesu alikuwa anayaangalia njiani wakati akiwa safarini kuelekea Yerusalemu! Katika maisha na utume wake wa hadhara, Yesu alibahatika kuwafunulia watu wema wa Mungu, kwa kuwaganga na kuwatibu wale wote waliokuwa chini ya utawala wa shetani! Akiwa njiani alitambua kwamba, saa yake imewadia ya kung’oa mzizi wa ubaya na dhambi kwa njia ya Msalaba.

Baba Mtakatifu anasema, hata waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kumfuasa Kristo, lakini mwaliko huu ni mkubwa zaidi kwa Makardinali wapya, wanaoitwa na Kristo Yesu kufuata nyayo zake kwa dhati kabisa, huku wakiwa makini katika utekelezaji wa malengo ya Kristo mwenyewe. Wanaitwa na kutumwa kuwa ni wahudumu wa ndugu zake Kristo; wanahamasishwa kusimama kidete dhidi ya dhambi za ulimwengu na madhara yake kwa watu wa nyakati hizi. Makardinali wapya wawe na ujasiri wa kutembea mbele ya familia ya Mungu, huku wakikaza macho yao kwenye Msalaba wa Kristo na Ufufuko wake kwa wafu! Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaweka Makardinali wapya chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili kwamba, Roho Mtakatifu aweze kusaidia kuwaweka karibu zaidi na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili kweli maisha yao, yaweze kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

29/06/2017 07:00