2017-06-29 15:48:00

Kardinali George Pell arejea Australia kujibu tuhuma zinazomkabili!


Vatican imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa kutoka Mahakama ya Australia inayomtaka Kardinali George Pell, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya uchumi kufika mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili kuhusiana na nyanyaso zilizotendwa na baadhi ya Wakleri wakati wa uongozi wake nchini Australia, miaka kadhaa iliyopita. Kardinali Pell akitambua mashitaka dhidi yake, sheria, kanuni na taratibu, ameamua kurejea nchini kwake Australia ili kufuatilia kwa karibu zaidi hii kesi, ili iweze kuendeshwa katika haki wakati huu ukweli juu ya shutuma hizi unapotafutwa.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kupata ya taarifa rasmi kutoka kwa Kardinali Pell, amempatia Likizo bila malipo ili kwenda nchini Australia kujitetea mwenyewe. Kipindi chote ambacho Kardinali Pell atakuwa nchini Australia, Sekretarieti ya uchumi itaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake katika masuala ya kawaida “donec aliter provideatur” “hadi pale itakapoamriwa vinginevyo”. Baba Mtakatifu Francisko ametumia nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Kardinali Pell kwa mchango wake mkubwa katika kipindi cha miaka mitatu alichofanya kazi kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican.

Amejitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake katika uaminifu mkubwa na kwamba, anamshukuru sana kwa mchango wake katika mageuzi ya shughuli za kiuchumi na uongozi mjini Vatican pamoja na ushiriki wake katika Baraza la Makardinali washauri. Vatican inaheshimu sheria za Australia na ina matumaini kwamba, haki itaweza kutendeka. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Pell amekuwa daima akishutumu vitendo vyote vya nyanyaso za kijinsia na kwamba, kwa miaka iliyopita ameshirikiana kwa karibu zaidi na  Serikali ya Australia. Ameshirikiana kwa karibu sana na Tume ya Kipapa ya kulinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Kama Askofu wa Australia alianzisha mtindo, sheria na taratibu za kuwalinda watoto pamoja na kuwasaidia waathirika wa nyanyaso za kijinsia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.