2017-06-28 14:45:00

Utume wa Khalifa wa Petro ni kazi ya Roho Mtakatifu


Huu ni mwaka wa tano wa utume wa Baba Mtakatifu Francisko akiwa Khalifa wa mtume Petro. Waamini popote duniani wanapounganikana naye kuadhimisha sikukuu ya watakatifu Petro na Paulo, wanatambua kuwa ni sehemu hai ya Kanisa ambalo analiongoza. Baba Mtakatifu ni Khalifa wa mtume Petro, mtumishi wa watumishi wa Bwana, kiongozi wa nchi ya Vatican, na zaidi sana ni kiongozi ambaye kwa upendo anawaimarisha ndugu zake katika imani. Askofu mkuu Julius Janusz, Balozi wa Vatican nchini Slovenia, akitoa mahubiri wakati wa kuadhimisha Sikukuu ya watakatifu Petro na Paulo, katika Kanisa kuu la Jimbo kuu la Lubiana, amewaasa waamini kutambua utendaji wa Roho Mtakatifu kupitia nafasi ya Khalifa wa mtume Petro.

Kumekuwa na maandishi mengi juu ya utume wa Baba Mtakatifu, na kwa namna ya pekee kuhusu shughuli, vipaumbele na namna ya utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Kuna wanaojiona wana haki na uhuru wa kuchambua na kuonesha kasoro kwenye utume wake. Watu hawa wanaonekana kutoamini, kutotambua, na kutopokea ukweli kwamba Baba wa mbinguni ndiye aliyemfunulia Petro ukweli wa mwanae kuwa ni Kristo, mwana wa Mungu aliye hai. Mvuvi wa hali ya kawaida kabisa, akaweza kutambua fumbo na siri kubwa ya umungu wa Kristo: heri wewe Simoni mwana wa Yona, kwa maana hakuna binadamu yeyote aliyekufumbulia jambo hili, ila Baba yangu aliye mbinguni (Rej., Mathayo 16:17).

Wale wanaojionesha kukosoakosoa utume wa Khalifa wa mtume Petro, ni kati ya watu wasioelewa hata chanzo na misingi ya nafasi hiyo. Ni kama mtu ambaye hesabu na fizikia kwake ni mama mkwe, halafu anajiweka kifua mbele kuanza kuelezea kanuni ya Einstein kuhusu jinsi vitu vinaweza kusafiri bila kufuata muda na nafasi. Askofu mkuu Julius Janusz anatahadharisha waamini kutohadaika na maneno maneno ya watu wasiofahamu ukweli wa mambo, watu wasiowacha Mungu wala hawafuati mapenzi ya Mungu kwa utii, bali wanatafuta kugawanya waamini na jamii kwa ujumla. Hii ni tabia ya kiibilisi, kwani Ibilisi ndiye baba wa udanganyifu, baba wa chuki, baba wa kutawanya badala ya kuunganisha.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na watoto katika moja ya parokia za Jimbo kuu la Roma, anajibu swali kuhusu kama amewahi kudhania kuwa Khalifa wa mtume Petro akisema: Kristo ndiye anayechagua nani awe Baba Mtakatifu kwa kipindi fulani, kama vile Askofu au Padre anapopewa utume fulani, na anayepewa jukumu hilo anapaswa alipokee na kuutimiza wajibu wake kwa upendo na imani. Askofu mkuu Julius Janusz anasema, Baba Mtakatifu Francisko hakujichagua kuwa Khalifa wa mtume Petro, kwani hiyo ni kazi ya Roho Mtakatifu.

Waamini wanaalikwa kuwa makini na ndumila kuwili katika jamii ya leo. Kuna watu wanajifanya kuwa wakristo lakini ni mbwa mwitu wanaotafuta kuwagawanya na kuwashambulia kondoo wa Bwana. Mfano nchini Slovenia hivi karibuni, kuna mwanasiasa aliyejitambulisha kuwa ni mkristo mkani-Mungu. Askofu mkuu Julius Janusz anasema, hakuna kitu kama hicho, sababu mtu au anakuwa mkristo sababu anamwamini Mungu au anakuwa mkani-Mungu sababu hamwamini. Haiwezekani kuwa na utambulisho wa vyote viwili kwa wakati mmoja. Huo ni undumila kuwili, uibilisi wa makusudi ili kuwahadaa na kuwapoteza watu. Askofu mkuu Julius Janusz kawaalika waamini kuendelea kumuombea Baba Mtakatifu ili atimize vema utume wake akiwa Khalifa wa mtume Petro kwa ujasiri na kwa maongozi ya Kristo Mwenyewe.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.