2017-06-28 14:28:00

Unafikiwaje Mkataba wa kijamii kimataifa kwa ajili ya wahamiaji!


Jukwaa la kimataifa kwa ajili ya wahamiaji na maendeleo linakutana Berlin kwenye mkutano wa kumi, kuanzia tarehe 28 – 30 Juni, 2017, katika harakati za majadiliano ya kutafuta ushirikiano wa kimataifa ambapo kwa sasa mwelekeo ni kutafuta Mkataba wa kijamii kimataifa kwa ajili ya wahamiaji na maendeleo. Katika mkutano huo, Vatican inawakilishwa na Padre Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, idara ya wakimbizi na wahamiaji katika Baraza la kipapa la huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu.

Akichangia hoja wakati wa majadiliano, Padre Michael Czerny anasema, ili Jamii ya Binadamu itoe jibu mahususi kufuatia changamoto ya wahamiaji, haina budi kutazama kwa umakini mambo mawili. Kwanza ni kujenga utamaduni wa kuwapokea, kuwalinda, kuwawezesha na kuwasaidia kuwa sehemu shirikishwa katika jamii. Pili, ni kuhakikisha kwamba hatua hizo zinawasindikiza wakati wote wa safari yao kuanzia nchi zao mahalia, nchi wanamopita, nchi wanakoelekea na kupata hifadhi, na kadiri inavyowezekana katika harakati za kurudi katika nchi zao.

Suala la huduma kwa wahamiaji linapaswa kuwa na utaratibu mzuri, usalama, na uwajibikaji. Namna hii ya kukabiliana na changamoto ya wahamiaji itaenda mbali zaidi ili kuepuka kushughulikia masuala kwa dharura, na badala yake kujenga mfumo wa maendeleo endelevu ya binadamu. Mfumo utakaoendana na heshima kwa utu wa binadamu, kiasi cha kuhakikisha haki ya kubaki katika nchi mahalia kuliko mahangaiko ya kuhama kwenda kutafuta hifahdi ugenini. Mfumo huo uwe na mwelekeo wa kuhangaikia mafao ya wengi na sio kundi fulani la watu. Wajibu huu ni wajibu wa kila nchi, wajibu wa kila taifa kuhakikisha raia wake wanapata haki zao msingi, kufuatana na mfumo mzuri wa utawala na maendeleo. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II anafundisha kwamba, ni haki ya msingi kuishi kwenye nchi mahalia, lakini haki hiyo huwa thabiti pale ambapo sababu zinazopelekea watu kuhama ama kukimbia nchi zao zinapodhibitiwa vizuri.

Wahamiaji wengi wanaokimbia nchi zao kutoka Afrika, ndio tumaini la Bara la Afrika, kwani ni vijana wenye nguvu, kalama, na ujasiri. Ni wakati wa kufifia kwa matumaini ya kimaendeleo kwa Bara la Afrika, na wakati huo huo vijana hao wanaonusurika na hatari za safari, wanatia nanga kwenye fukwe za nchi za Ulaya bila matumaini ya mafanikio yao kwa siku za usoni. Ni kama wanaelekea kupoteza lulu waliyoiacha nyumbani kwao, na hawakipati kipande cha keki walichokikimbilia barani Ulaya. Hata hivyo ukweli unabaki kwamba, ili wabaki kwenye urithi wa lulu zao barani Afrika, ni lazima wajisikie huru na amani kubaki katika nchi zao.

Katika maeneo ambako wahamiaji wanapata hifadhi, tayari kuna watu wanaishi katika hali ya umaskini. Hatari ni kuhangaikia upande mmoja na kusahau upande mwingine. Padre Michael Czerny anasema, kanuni ya nusu kwa nusu, hamsini zako hamsini zangu, itiliwe maanani ili kuhakikisha malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu yanafikiwa. Malengo hayo yanataka kuhakikisha kwamba nchi zinazoendelea zinawezeshwa kujikwamua kutoka kwenye hali hafifu, lakini wakati huo huo nchi zilizoendelea zinadumisha huduma stahiki kwa mahitaji yao msingi. Kwa mantiki hiyo, jumuiya zinazowakirimu wahamiaji, zitoe huduma na kuwahangaikia wahamiaji hao, bila kuwasahau maskini wa jumiya zao ambao wamekuwa sehemu ya jumuiya hizo kabla ya changamoto ya wahamiaji.

Kwa mwenendo huo, kutaepukwa kinzani kati ya wahamiaji na wakazi ambapo wahamiaji wanapata hifadhi. Chuki nyingi zimekuwa zikionekana kutoka kwa wakazi wa jumuiya ambako wahamiaji wanapata hifadhi, sababu ya hofu ya kupoteza kile walicho nacho. Kumbe ni lazima kuhudumia mahitaji ya chakula, mavazi, maji safi na salama, malazi, huduma za afya na elimu, mawasiliano na usalama kwa pande zote mbili, yaani wahamiaji na wakazi walio kwenye hali ya umaskini. Hivyo mfuko wa dharura utakuwa umetenda haki kwa wote, na kudumisha amani, upendo na udugu kati ya wanadamu kokote duniani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema: ukosefu wa uwiano kati ya watu unasababishwa na vita, umaskini, uhamiaji na watu wanatafuta jukwaa la kujieleza na kusikilizwa mahangaiko na hofu zao, sababu wanaona rasilimali za dunia zinawanufaisha wachache tu. Padre Michael Czerny anasema: mapambano ya kutafuta maendeleo endelevu kwa jamii ya binadamu, yanahitaji sana ushirikishwaji hai wa kila mmoja katika jamii anamoishi. Hii ina maanisha ni lazima hata wahamiaji washirikishwe vizuri katika jamii walimopata hifadhi, ili wawe sehemu ya kujenga maendeleo kiuchumi, kisiasa, kijamii, na kitamaduni katika jamii walimojikuta, kwa mtazamo wa kuwajengea pia fursa ya kurudi katika nchi zao mahalia. Pamoja nao, maskini wa jamii hifadhi wahusishwe pia kwa maendeleo endelevu ya jamii yao.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

   

 








All the contents on this site are copyrighted ©.