2017-06-28 15:25:00

Papa Francisko: Matumaini ya Kikristo ni nguvu ya mashuhuda wa imani!


Yesu aliwaambia mitume wake kwamba, anawatuma kama kondoo kati ya mbwamwitu, hivyo walipaswa kuwa na busara kama nyoka na wapole kama hua, kwani huko duniani, watakiona cha mtema kuni! Kutakuwa na kinzani na wengi watawachukia kwa sababu ya jina lake. Lakini, aliwakumbusha kwamba, wale watakaovumilia hadi mwisho, hao ndio watakaookoka. Matumaini ya Kikristo ni nguvu ya mashuhuda na waungama imani. Yesu alipowachagua na kuwatuma wafuasi wake, hakuwahakikishia mafanikio ya chapuchapu kama maji kwa glasi!

Kristo Yesu, aliwaonya na kuwaambia kwamba, utangazaji, ushuhuda na ujenzi wa Ufalme wa Mungu una magumu na changamoto zake kwani watachukiwa kwa sababu ya jina lake. Hili ni jambo la kushangaza sana kwani Wakristo wanapenda kwa asili, lakini daima wanachukiwa sana. Imani thabiti inashuhudiwa katika mazingira kinzani na hatarishi! Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Wakristo ni watu wanaopambana na mawimbi makali ya maisha na kwamba, ulimwengu umejeruhiwa sana na uwepo wa dhambi. Hali hii inashuhudiwa kutokana na ubinafsi uliokithiri sanjari na ukosefu wa haki msingi za binadamu hasa kwa wafuasi wa Kristo, kwani wao wanajitahidi kukita maisha yao katika mantiki ya matumaini yaliyofunuliwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 28 Juni 2017 kama sehemu ya mwendelezo wa katekesi kuhusu matumaini ya Kikristo! Changamoto ya kwanza inayotolewa na Kristo Yesu kwa wafuasi wake ni ufukara kwa kujivua na malimwengu, ili kuweza kutumia rasilimali, utajiri na mapaji ambayo Mkristo amekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mkristo anayependa kumezwa na utajiri wa duniani anakwenda kinyume na mfano wa maisha uliotolewa na kushuhudiwa na Kristo Yesu mwenyewe.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hija na maisha ya Wakristo hapa duniani inapaswa kufumbatwa katika upendo na kuondokana na kishawishi kinachoweza kuwatumbukiza katika: vita, machafuko na tabia ya kulipizana kisasi! Daima wakumbuke kwamba, wanaitwa na kutumwa na Kristo Yesu kama kondoo kati ya mbwamwitu! Amani ndiyo silaha yao madhubuti, daima wakijitahidi kujivika fadhila ya busara na hekima mintarafu mwanga wa Injili. Wajitahidi kushinda ubaya kwa kutenda wema! Nguvu na jeuri ya Wakristo ni Injili ya Kristo mwenyewe katika kipindi cha shida na karaha kwani wanatambua kwamba, Yesu daima yupo pamoja nao! Mateso, dhuluma na nyanyaso ni sehemu ya vinasaba vya Injili kwani hata Kristo Yesu mwenyewe alitendwa jeuri, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kujenga na kudumisha matumaini na kamwe wasidhani hata siku moja kwamba, Kristo Yesu anaweza kuwaacha wamezwe na mawimbi makubwa ya bahari ya mateso, dhuluma na nyanyaso, kwani wao wanayo thamani kubwa sana mbele ya macho yake. Mateso na mahangaiko yao, daima yako mbele ya uso wa Mwenyezi Mungu anayewaona na kuwapigania kwa wakati wake. Mwenyezi Mungu ambaye yuko kati ya watu wake ana nguvu zaidi kuliko ubaya, magenge ya kigaidi na uvuli wa mauti unaowanyanyasa wale waliokata tamaa na kuonewa na wenye nguvu hapa duniani. Mwenyezi Mungu daima anasikiliza kilio cha damu ya Abeli kinachosikika kutoka ardhini!

Kutokana na mwelekeo huu, Wakristo hawana budi kuwa ni sehemu ya wale wanaoteswa na kamwe wasiwe ni watu wanaowatesa wengine; wenye kiburi, bali wanyenyekevu na wapole wa moyo! Wasiwe ni ”wambeya, wazandiki na watu wanaopepeta midomo” dhidi ya jirani zao, bali vyombo na mashuhuda wa Injili ya ukweli, uaminifu na uadilifu. Uaminifu ni mtindo wa maisha ya Kristo Yesu, unaopata hitimisho lake katika ushuhuda ambao ni kielelezo makini cha wafuasi wa Kristo, hali ambayo imejionesha tangu mwanzo kabisa wa Kanisa.

Wakristo walikuwa tayari kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, lakini, hiki si kigezo cha juu kabisa cha utambulisho wa Mkristo! Badala yake ni amri ya upendo kwa Mungu na jirani, kama anavyofafanua Mtakatifu Paulo katika utenzi wake wa upendo! Anasema, hata kama ”nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo si kitu mimi”. (Rej. 1Kor. 13: 3). Tabia ya kujinyonga haina tija wala mashiko machoni pa Mwenyezi Mungu anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Wakati huu, kuna idadi kubwa ya mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake, pengine kuliko wakati mwingine wowote wa historia ya maisha na utume wa Kanisa.

Wakristo wanapambana na changamoto zote hizi kwa nguvu ya matumaini ambayo kamwe hakuna mtu anayeweza kuwapokonya kwani inafumbatwa katika upendo wa Mungu uliomiminwa katika mioyo ya waamini kwa njia ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake nguvu za kuweza kuwa kweli ni mashuhuda wa imani, kwa kuendelea kuishi matumaini ya Kikristo yanayomwilishwa katika upendo unaotekelezwa kila siku ya maisha!

Na Padre Richard A, Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.