2017-06-28 14:15:00

Msimamo wa Vatican juu ya mpango wa afya ya uzazi wa Umoja wa Mataifa


Pamoja na majadiliano ya uwazi na matunda ya ushirikiano kwa wajumbe wengi wa kimataifa kuhusu mipango na utekelezaji wa pamoja kutoa misaada ya dharura kwa wahanga wa mahitaji msingi ya binadamu sehemu mbali mbali duniani, makubaliano ya pamoja na uwiano wa kukabiliana na changamoto hizo vimekuwa vigumu sana kwa jumuiya ya kimataifa.

Kumekuwa na hatua kubwa sana kwenye baadhi ya vipengele mfano katika kukabiliana na baa la njaa kwa kuhakikisha usalama wa chakula, kwa upande mwingine kumewekwa kipengele kuhusu afya ya uzazi, kijulikanacho kama The Minimum Initial Service Package. Jicho likiwa kavu na bila kukwapua hata utepe wa kope, ndivyo anavyofunguka Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss, akielezea msimamo wa Vatican kuhusu baadhi ya maamuzi ya vikao katika kukabiliana na changamoto za dharura kwa mahitaji msingi ya binadamu maeneo kadhaa duniani.  

The Minimum Initial Service Package ni shughuli kadhaa zinazopewa kipaumbele na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani, UNFPA, ambapo inatolewa mikoba 13 ya afya ya uzazi iliyoandaliwa maalumu kwa ajili ya akina mama na wasichana wenye umri wa kubemba mimba. Baadhi ya mikoba hiyo ina nyenzo za utoaji mimba. Mfano mkoba ujulikanao kwa namba 10 (KIT 10), una vacuum extractor, chombo kinachotumika sana kutoa mimba na kina madhara makubwa kwa afya za akina mama.

Askofu mkuu Ivan Jurkovic anasema, huduma ya afya haiwezi kutolewa dhidi ya uhai wa wanyonge au watoto ambao bado hawajazaliwa, kwa madai ya kujali na kuchagua afya ya mmoja kuliko uhai wa mwingine. Binadamu wote ni sawa, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanayo haki ya kuishi bila kujali hatua ya maisha ki umri au kihali. Vatican inatambua hatari za kiafya kwa akina mama na watoto, mazingira magumu na mahitaji ya binadamu kama chakula katika maeneo yenye changamoto kadha wa kadha, hata hivyo haikubaliani na mipango inayodai kujali watu kwa kushabikia na kuwezesha utoaji mimba.

Kwa msimamo huo, Ujumbe wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, nchini Uswiss, haukubaliani na shughuli za The Minimum Initial Service Package, sababu ndani yake kuna shughuli za utoaji mimba. Akina mama na watoto katika maeneo hayo, tayari wamo kwenye majanga makubwa ya baa la njaa, afya hafifu, ubakwaji, na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. Katika msimamo wake Vatican inasisitiza mambo mawili: Moja, utoaji mimba wala fursa zozote zenye mwelekeo kama huo haviwezi kutambuliwa kana kwamba ni afya ya uzazi au huduma kwa afya ya uzazi na; Pili, jinsia itambulike kuwa ni suala lenye utambulisho msingi kibaiolojia, na kwa misingi hiyo hiyo ya kibaiolojia zitambuliwe tofauti kati ya mwanamume na mwanamke, sio zaidi wala sio pungufu. Askofu mkuu Ivan Jurkovic, amesisitiza kwamba msimamo huo wa Vatican kuhusu suala la afya ya uzazi na jinsia, uwekwe kwenye kumbukumbu kwa ajili ya rejea kwa siku za usoni.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.