2017-06-28 15:44:00

Maaskofu wakuu 36 kupewa Pallio Takatifu, kati yao 8 ni kutoka Afrika


Mwenyezi Mungu wa milele anapenda kulipatia Kanisa lake furaha kubwa ya kuadhimisha Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume, miamba wa imani, kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni. Hii ni changamoto kwa Kanisa kufuata mafundisho yao kikamilifu. Hii inatokana na ukweli kwamba, wao ndio waliokuwa mitume wa kwanza waliowafundisha waamini kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu anayetawala pamoja na Roho Mtakatifu, milele yote!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 28 Juni 2017 amewataka waamini kuwakumbuka na kufuata mifano bora ya maisha na ushuhuda uliotolewa na miamba hii ya Injili, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa kweli ni mashuhuda amini na wadumifu wa Kristo katika maisha yao ya kila siku! Wakristo wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini na ushuhuda unaofumbatwa katika kutenda mema, kutekeleza dhamana na wajibu wa kila siku pamoja na kumwilisha Injili ya upendo kwa Mungu na jirani! Waamini wawe na ujasiri wa kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kiinjili!

Katika Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican majira ya asubuhi, atabariki Pallio takatifu kwa ajili ya Maaskofu wakuu wapya 36 kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kati yao kuna Maaskofu wakuu 8 kutoka Barani Afrika. Taarifa zinaonesha kwamba, Maaskofu wakuu 4 hawataweza kuhudhuria Ibada hii kutokana na sababu mbali mbali. Maaskofu wakuu kutoka Barani Afrika ni:

Askofu mkuu Antony Muheria kutoka Jimbo kuu la Nyeri, Kenya.

Askofu mkuu Inàcio Saure, kutoka Jimbo kuu la Nampula, Msumbiji.

Askofu mkuu Paul Desfarges, kutoka Jimbo kuu la Algeria, Algeria.

Askofu mkuu Michael Didi Adgum Mangoria, Jimbo kuu la Khartoum, Sudan, K.

Askofu mkuu Fridolin Ambongo Besungu, Jimbo kuu la Mbandaka, DRC.

Askofu mkuu Faustin Ambassa Ndjodo, Jimbo kuu la Garoua, Cameroon.

Askofu mkuu Goetbe Edmond Djitangar, Jimbo kuu la N’Djamena, Chad.

Kwa upande wake Kardinali Angelo Comastri, Mwakilishi wa Baba Mtakatifu katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafanyakazi wa Vatican, amewakumbusha kwamba, wamebahatika kutekeleza majukumu yao ya kazi mahali ambapo, miamba ya imani, Mitume Petro na Paulo, waliyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa na baada yao, kumekuwepo na umati mkubwa wa Wakristo wanaoendelea kusadaka maisha yao. Si kwamba, hawa walikuwa ni watu wabaya sana humu duniani, ila tu kwa sababu walikuwa ni wafuasi aminifu, watu wema na wenye haki. Ni mitume ambao wamelipa gharama ya upendo kwa kumwaga damu yao, ili Kanisa liweze kuendelea kucharuka katika maisha ya utume wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.