2017-06-27 08:25:00

Patriaki Youssef Absi achaguliwa kuongoza Kanisa Mashariki ya Kati!


Patriaki Youssef Absi aliyechaguliwa hivi karibuni kuwa Patriaki mpya wa Kanisa la Kigiriki la Kikatoliki huko Antiokia na Mashariki yote, amemwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko akiomba kupewa umoja wa Kikanisa baada ya maadhimisho ya Sinodi yaliyofanyika kuanzia tarehe 19- 23 Juni 2017. Patriaki Youssef Absi katika barua yake anasema, anatambua fika kwamba, hastahili kupewa nafasi hii, ili kumrithi Patriaki Gregori wa III.

Lakini kwa furaha na matumaini makubwa, anapenda kumjulisha Baba Mtakatifu Francisko uchaguzi uliofanywa na Sinodi kama kielelezo makini cha umoja wa Kanisa unaoonekana na Kanisa Katoliki pamoja na Kanisa la Kigiriki la Kikatoliki la Antiokia na Mashariki yote. Anamtambua kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kiongozi mkuu wa Kanisa la Kristo duniani.

Patriaki Youssef Absi anakaza kusema, Kanisa hili limekuwa aminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kama kielelezo makini cha umoja wa Kikanisa, kihistoria, dhabiti na katika Sinodi. Kwa niaba ya Kanisa hili linalopenda na kuthamini  utume wa Baba Mtakatifu Francisko katika shughuli za kichungaji, kiekumene na kiulimwengu, anapenda kuonesha uaminifu wake yeye! Anakaza kusema, ameamua kuchagua jina la Youssef na kwamba, ataendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuendeleza amana ya maisha ya kiroho kutoka katika Makanisa ya Mashariki na kwamba, ataendelea kuimarisha umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa kuonesha uaminifu wake kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, anamwomba, Baba Mtakatifu Francisko apokee ombi lake kwa njia ya Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.