2017-06-27 14:52:00

Papa Francisko anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu Jumanne, tarehe 27 Juni 2017 yaliyowashirikisha Makardinali na Maaskofu wanaoishi na kufanya utume wao mjini Roma, amewashuruku kwa umoja katika sala, anapomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu, ili aweze kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu! Baba Mtakatifu anasema, Jubilei ni kipindi cha kuomba toba na msamaha wa dhambi; ni muda muafaka wa kuchuchumilia wongofu wa ndani, udumifu katika imani, matumaini na mapendo. Anawashukuru viongozi wote wa Kanisa waliojumuika pamoja katika Ibada hii ya Misa anapomshukuru Mungu kwa Jubilei ya miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu. Amewaombea wote neema na baraka katika huduma ya Kanisa!

Katika mahubiri yake anasema, baada ya Abramu na Lutu kutengana kila mtu akashika “hamsini zake”, Abramu alipata nafasi ya kuzungumza na Mwenyezi Mungu na mazungumzo yao yalijikita katika mambo makuu matatu: “Inua sasa macho yako”, “Ukatazame kutoka hapo ulipo” “maana nchi yote uionayo sasa nitakupa wewe na uzao wako hata milele”. Kwa ufupi kabisa, Mwenyezi Mungu alimwambia Abramu: Inuka, Tazama na Tumainia! Mwenyezi Mungu anamtaka Abramu kuanza safari katika maisha yake, daima atakuwa ni “kiguu na njia” na hema litakuwa ni mahali pake pa kupumzikia.

Mwenyezi Mungu alimwambia Abramu, tazama upande wa Kaskazini na Kusini, Mashariki na Magharibi, mwaliko wa kujenga madaraja ya kukutana na watu na kamwe si ukuta unaokuwa kikwazo. Mwenyezi Mungu anamtaka Abramu kuwa ni mtu wa matumaini kwani ataweza kutekeleza ahadi zake kwa wakati muafaka, licha kuwa mkewe Sarah alikuwa mgumba na tayari alikuwa na umri mkubwa, lakini huyu ndiye ambaye Mwenyezi Mungu alikuwa amemteua kutekeleza matumaini ya Mzee Abramu na kwamba, atampatia uzao ambao utakuwa kama mavumbi ya nchi, usiokuwa na idadi. Abramu akajenga matumaini kwa Mwenyezi Mungu na hii ikawa ni sehemu ya haki ambayo itafafanuliwa baadaye na Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Haya ni matumaini yasiyokuwa na ukomo wala ukuta!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Abramu aliitwa na Mwenyezi Mungu wakati alipokuwa anajiandaa kuanza kula pensheni ya maisha! Huu ni muda wa uzee unaonyemelewa na magonjwa pamoja na maumivu mbali mbali. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Mwenyezi Mungu hata kwa watu wa nyakati hizi anayewataka: kuinuka, kutazama na kutumainia, huku wakitoka kifua mbele katika kutekeleza utume wa Kanisa. Ni watu waliokula chumvi nyingi, wanao uzoefu na mang’amuzi, wanaoweza kuthubutu: kuinuka, kutazama na kutumainia. Mwenyezi Mungu anawaalika kuendelea kuota ndoto kama ilivyokuwa Simeoni na Anna wanaosimuliwa na Mwinjili Luka walipokuwa wanazungumza na Bikira Maria pamoja na Mtakatifu Yosefu. Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kuendelea kuwa na ndoto inayowashirikisha vijana wa kizazi kipya katika maisha na utume wao; kwa kuwashirikisha mang’amuzi, ili waweze kuendeleza unabii na utume wao. Hii ndiyo neema ambayo Baba Mtakatifu anawaombea viongzo wote wa Kanisa katika maisha na utume wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.