2017-06-27 07:49:00

Mbinu mkakati wa kimataifa wa kupambana na biashara ya binadamu!


Mnamo mwezi Septemba 2017, kutafanyika mkutano wa Umoja wa Mataifa jijini New York, kwa ajili ya kurejea kwa hali ya juu zaidi, ule mpango mkakati wa kupambana na biashara haramu ya binadamu, kwa kujikita katika kutetea haki msingi za binadamu na mahitaji ya wale wanaoathirika au wamewahi kuathirika na ukatili huo. Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, akichangia hoja katika kikao cha maandalizi wa mkutano  huo anaongelea uvunjwaji wa haki za binadamu na uteteaji wa haki kwa wale ambao ni wahanga wa biashara haramu ya binadamu.

Uvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu unaonekana kwenye msululu mzima wa biashara haram ya binadamu kama watumwa, kwa ajili ya ngono, kazi za shuruti, biashara ya viungo vya binadamu na unyonywaji. Biashara hii inaendekezwa pia na umaskini, ukosefu wa ajira, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji, mabadiliko ya tabia nchi, kinzani za kijamii na kisiasa. Hata hivyo mzizi wa haya yote ni kupoteza thamani na heshima kwa utu wa binadamu, kiasi cha kuwachukulia wengine kana kwamba ni bidhaa, amesisitiza Askofu mkuu Auza.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume Laudato sì, Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa Mazingira Nyumba ya wote, anasema: tabia ya kuharibu mazingira unapelekea kuchukulia wanadamu wengi kana kwamba ni vyombo vya kujitafutia faida binafsi, au kukidhi hamu ya tamaa binafsi kimapenzi na kisha kuvitupilia mbali. Askofu mkuu Auza anasema: iwapo Jumuiya ya kimataifa inanuia kweli kupiga vita biashara haramu ya binadamu, lazima itokomeze chanzo, ambacho ni utamaduni uliojengeka kwenye mioyo ya wafanya bishara husika, kudharau utu wa mwanadamu. Kwa waathirika wa biashara hii, haitoshi kutetea tu haki zao, bali ni muhimu kujihusisha moja kwa moja katika kuwakirimia mahitaji yao. Wapate uhuru wao, waponywe madonda yao kwa matibabu kifizikia, kisaikolojia, kiuchumi na kwa kuzingatia haki zao kisheria, anasema Askofu mkuu Bernadirto Auza.

Kwa namna hii watasaidiwa kuamka kutoka kwenye ndoto hiyo mbaya ya kutisha, na kuanza kuvumbua upya utu wao na pole pole kuweza kuamini tena kwamba wanaweza kuishi maisha bora. Vatican kupitia kikundi cha Mtakatifu Martha, na taasisi zake zingine mfano Talitha Kum na RENATE, zinazohusika na upigaji vita wa biashara haramu ya binadamu, imejizatiti katika kuwahudumia waathirika wa janga hilo ili kuwarudishia hadhi yao ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Askofu mkuu Bernadirto Auza anaialika Jumuiya ya kimataifa kuwekeza rasilimali kadiri iwezekanavyo kutokomeza kwanza kabisa utamaduni wa kudharau utu wa binadamu, ili kuweza kutokomeza bishara haramu ya binadamu.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.