2017-06-26 14:14:00

Suluhu ya ghasia DRC ni kupata Rais mpya kufikia Desemba 2017


Ili kuepuka mwendelezo wa hali tete na misigano ndani ya nchi, lazima uchaguzi mkuu ufanyike kufikia Desemba 2017, kadiri ya makubaliano ya Mt. Silvester. Wito huu umetolewa na Baraza la Maaskofu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Congo, tarehe 23 Juni 2017, wakati wa kuhitimisha mkutano wake mkuu uliokuwa ukifanyika mjini Kinshasa kuanzia tarehe 19 Juni 2017.  

 

Mwaka 2016 Rais Joseph Kabila alinuia kugombea mara ya tatu kinyang’anyilo cha urais, jambo ambalo ni kinyume na katiba ya nchi hiyo. Hali hii ilisababisha kuibuka kwa ghasia nchini Congo. Ndipo tarehe 31 Desemba 2016, yakafanyika makubaliano kati ya chama tawala na wapinzani, makubaliano yaliyosimamiwa na Baraza la Maaskofu Congo. Katika makubaliano hayo yajulikanayo kama makubaliano ya Mt. Silvester, Rais Joseph Kabila alipewa mwaka mwingine zaidi wa uongozi, na kuandaa kwa utulivu uchaguzi mkuu kufikia mwisho mwa mwaka 2017. Katika makubaliano hayo aliteuliwa Waziri mkuu kutoka upinzani, Bwana Etienne Tshisekedi, na kuundwa Baraza la kitaifa litakalofuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo. Mwezi mmoja baadae Bwana Etienne Tshisekedi alifariki dunia, kukawa na sintofahamu ndani ya vuguvugu la vyama vya upinzani nchini Congo, na hivyo harufu mbaya ya ghasia kuibuka tena imeanza kuchafua hali ya hewa nchini Congo.

Maaskofu nchini Congo wameandika Waraka unaoongozwa na kauli mbiu: nchi inaelekea pabaya sana, Wakongo simameni. Katika waraka huo, maaskofu wa Congo wanaelezea jinsi uchumi wa nchi unavyozidi kudorora, usalama wa raia na mali zao mashakani, na machafuko ya kisiasa, mambo ambayo hivi karibuni hata Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva Uswiss, aliyagusia akilialika Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki Msingi za Binadamu kuingilia kati uvunjwaji wa haki msingi za binadamu nchini Congo. Ukuaji wa uchumi nchini Congo kwa miaka ya nyuma ulikuwa wa kasi sana, lakini kwa sasa inaonekana kubaki kama historia, kwani rushwa na matumizi mabaya ya rasilimali za umma vimepelekea myumbo mkubwa wa uchumi, na wanaoumia zaidi ni familia za watu wa Congo, jambo linalopelekea pia vijana wengi kujiunga na ujangili na vikundi vya mapigano ya silaha. Malimbikizo ya mishahara ambayo haijalipwa kwa miezi mingi, ukosefu wa mlo ndani ya familia nyingi, na upungufu wa maji na umeme kwenye miji mingi ni kati ya mambo yanayowatesa “Bana ba Congo”.

Usalama wa nchi ya Congo umekuwa mdogo sana, na mahitaji msingi ya raia wa nchi hiyo yanapeperushwa kama tiara kwenye kimbunga kikali. Kwa maeneo ya kanda ya Kasai hali ni mbaya zaidi, ambapo kuna mapigano makali kati ya jeshi la serikali na kikundi cha waasi. Miezi tisa tangu machafuko yaanze nchini humo, takwimu zinaonesha wamefariki watu 3,383 na 30,000 wametoroka kutafuta hifadhi kwenye kambi za wakimbizi nchini Angola. Kanisa pia limeathirika sana kwani parokia 60 zimevamiwa, na vijiji 20 vimebomolewa makazi hakuna na hakuna uwezekano wa kutoa huduma za kiroho maeneo hayo, watoto wanatekwa na wengine kuuwawa. Ishara wazi ya baadhi ya “Bana ba Congo” kutumia vibaya madaraka au nafasi walizo nazo katika jamii kwa kuwaonea wanyonge, badala ya kutafuta manufaa ya wengi. Maaskofu Congo wanaialika serikali ya Rais Jospeh Kabila kukomesha ghasia hizo.

Maaskofu wa Congo wanasisitiza kwamba ili kuondokana na hali mbaya iliyopo na kurudisha usalama na maendeleo nchini Congo, ni lazima uchaguzi mkuu ufanyike kufikia mwisho wa mwaka 2017, vinginevyo hali inaweza kuwa mbaya zaidi. Kwa upande wao maaskofu, wakiongozwa na Injili ya Kristo pamoja na mafundisho jamii ya Kanisa, wanautambua wajibu wao na wameanza kuhamasisha utekelezaji wa makubaliano ya Mt. Silvester, ambapo kutakuwa na maandamano ya amani nchi nzima yakiongozwa na vikundi takribani 200 vya kitume, kisha tarehe 30 Juni 2017, kuwa siku ya mfungo na sala kwa taifa zima.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.