2017-06-26 09:28:00

Papa Francisko aguswa na maafa makubwa yaliyotokea nchini China!


Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 25 Juni 2017 aliyaelekeza mawazo yake nchini China, ili kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu walioathirika kutokana na kufunikwa na maporomoko ya ardhi yaliyotokea, Jumamosi, tarehe 24 Juni 2017 kwenye Kijiji cha Xinmo na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu na mali zao.  Nyumba 62 zimefunikwa kwa kifusi na zaidi ya watu 100 hawajulikani mahali waliko! Baba Mtakatifu anawaombea marehemu pumziko la milele na faraja kwa majeruhi na wale wote waliopoteza makazi yao. Mwenyezi Mungu aendelee kuwafariji wale wote wanaotoa msaada kwa waathirika na kwamba, yuko karibu na wananchi wa China katika kipindi hiki kigumu!

Baba Mtakatifu Francisko amegusia pia tukio la kihistoria la kutangazwa kwa Askofu mkuu Teofilius Matulionis kuwa Mwenyeheri katika Ibada iliyoongozwa na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu huko, Vilnius, nchini Lithuania. Askofu mkuu Teofilius Matulionis aliuwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani ya Kikristo kunako mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 90. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ushuhuda uliotangazwa na kuoneshwa na Mwenyeheri Askofu mkuu Teofilius Matulionis, aliyethubutu kusimama kidete kutetea imani, utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwatia shime viongozi wa Kanisa, waamini na mahujaji kutoka Kanisa la Kigiriki la Kikatoliki huko nchini Ukraine na Bielorussia wanaoadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu Mtakakatifu Yosefati alipotangazwa kuwa Mtakatifu. Baba Mtakatifu tangu sasa anapenda kuungana nao kiroho katika kuadhimisha Liturujia Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawaombea wote hawa ujasiri wa ushuhuda wa imani ya Kikristo na amani kwa nchini ya Ukraine ambayo bado inapitia kipindi kigumu cha historia na maisha yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.