2017-06-26 15:25:00

Dr. Joachim von Braun ateuliwa kuwa Rais wa Taasisi za Kipapa!


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amemteua Dr. Joachim Von Braun kuwa Rais mpya wa Taasisi za Kipapa za Sayansi. Alizaliwa tarehe 10 Julai 1950 huko Brakel, Ujeruman. Alisoma katika vyuo mbali mbali huko nchini Ujerumani na kufaulu kujipatia Shahada ya uzamivu katika masuala ya tafiti na baadaye akapewa dhamana ya kufundisha Chuo kikuu cha Kilimo cha Gottingen. Amewahi kufundisha pia vyuo vikuu vya Kiel na Bonn nchini Ujerumani. Ni mwandishi maarufu wa vitabu na makala kuhusu maendeleo na uchumi wa kimataifa; rasilimali asilia, mapambano dhidi ya umaskini, sera za mabadiliko chanya ya kisayansi, teknolojia kama chombo cha kumsaidia mwanadamu kupiga hatua zaidi ya maendeleo sanjari na biashara ya kimataifa!

Dr. Joachim Von Braun ni kati ya mabingwa wanaotambulikana na Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani sanjari na sera makini zinazoweza kutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa ili kuokoa mamilioni ya watu wanaokufa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Amewahi kuwa ni Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kimataifa kuhusu Sera za Chakula “International Food Policy Research Institute, Ifpri.” yenye Makao yake makuu Jijini Washington DC., huko Marekani kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2009. Kwa miaka mingi amekuwa ni mtaalam mshauri wa siasa ya uchumi kwa nchi nyingi kutoka Afrika na Asia.

Kuanzia mwaka 2009 hadi sasa ni Mkurugenzi wa Kituo cha tafiti za maendeleo ya kiuchumi na kijamii na ni Jaalimu aliyebobea katika masuala ya uchumi na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika Chuo Kikuu cha Bonn, nchini Ujerumani. Ni Rais wa Baraza la “Bio Economy” la Serikali ya Ujerumani na mtaalam na mshauri katika mabaraza mbali mbali katika Umoja wa Ulaya. Hivi karibuni alikuwa ni kati ya wawezeshaji wakuu katika Jukwaa la Uchumi Kimataifa huko, Davos na kwamba, ameshiriki mara nyingi katika makongamano na mikutano ya kimataifa iliyokuwa inaandaliwa na Umoja wa Mataifa pamoja na taasisi mbali mbali za kimataifa.

Kimsingi Dr. Joachim Von Braun Rais mpya wa Taasisi za Kipapa za Sayansi ni mtaalamu aliyebobea katika masuala ya maendeleo endelevu ya binadamu; uchumi na kilimo na kwamba, kuanzia mwaka 2012 aliteuliwa kuwa ni mwanachama wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi. Anaheshimika sana katika masuala ya usalama na uhakika wa chakula duniani, changamoto inayovaliwa njuga kwa sasa na Jumuiya ya Kimataifa, ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watu wanaofariki dunia kutokana na baa la njaa na utapiamlo. Mwishoni, Dr. Joachim Von Braun amemwoa Dr Barbara Von Braun na kubahatika kupata naye watoto watatu, matendo makuu ya Mungu kwa maisha ya mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.