2017-06-24 13:41:00

Raia Kenya wachague viongozi waadilifu


Uchaguzi mkuu nchini Kenya unatarajiwa kufanyika tarehe 8 Agosti 2017, ambapo atachaguliwa Rais wa nchi na makamu wake, wabunge, na viongozi wa serikali za mitaa. Katika kinyang’anyilo cha urais wanaowania nafasi hiyo ni Rais wa sasa Bwana Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Bwana Raila Odinga. Utaratibu wa kuhesabu kura za ushindi ni kwamba anayeibuka kidedea kwenye nafasi ya urais lazima awe na zaidi ya asilimia hamsini (50%) ya kura zote, na wakati huo huo awe walau na asilimia ishirini na tano (25%) kwenye majimbo walau 24 ambapo Kenya ina majimbo 47 kwa sasa. Hii inafunua picha kwamba kweli Rais atakuwa chaguo la asilimia kubwa ya wananchi na sio raia wa upande fulani fulani tu nchini humo.

Katika harakati za kuelekea uchaguzi huo, Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Kenya limeandika barua ya kichungaji likiwaalika waamini na raia wema nchini humo kusimamia uchaguzi wa amani na wakuaminika, wakihakikisha wanachagua viongozi wachapakazi na waadilifu. Mafundisho jamii ya Kanisa yanaelezea kwamba: Binadamu ndiye msingi na lengo la masuala ya siasa na mfumo wa kijamii. Mwanadamu huyo huyo ameumbwa akiwa na akili na utashi, ili awajibike kwa uchaguzi anaopendelea na matendo anayofanya kwa ajili ya kutafuta maisha yenye manufaa na hadhi kwa kila mmoja na kwa jamii nzima.

Kanisa linatambua pia kwamba jamii yeyote katika mfumo wake wa utawala, inapata chachu kutoka kwa raia wenye uchaji wa Mungu na maadili mema, kiasi cha kuweza kukabiliana na changamoto zao na kutatua matatizo ndani ya jamii wanamoishi. Uthabiti wa maisha na utawala katika jamii hutegemea sana umoja wa watu katika jamii husika. Viongozi wa kila jumuiya huakisi tunu na maadili ya raia wa jumuiya wanayoiongoza. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema, uharifu na rushwa vinavyoonekana kati ya viongozi wa serikali ya nchi yao, vinawachafua wananchi wote wa Kenya, kwani inaashiria kuwa Kenya nzima ni taifa la ghasia na rushwa.

Kenya imekuwa na historia ya maumivu hivi karibuni kuhusiana na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008 kulitokea ghasia na machafuko nchini humo ambapo raia wengi walifariki au kuumizwa vibaya, kiasi cha waliokuwa viongozi wa serikali ya mseto kushtakiwa kwa makosa ya uhaini. Hawa ni pamoja na aliyekuwa Waziri mkuu Raila Odinga, Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka, Manaibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta, Musalia Mudavadi na William Ruto. Tayari wakati Kenya ilipokuwa ikielekea uchaguzi wa mwaka 2013, Kitengo cha Uchunguzi Kenya cha Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya uhaini, ICC, lilifungua kesi kuweka zuio la viongozi hao wasishiriki kwenye kinyang’anyilo, lakini mahakama kuu Kenya, baada ya kusikiliza kesi ilifutilia mbali ombi hilo.

Baada ya uchaguzi wa 2013 na Uhuru Kenyatta kuibuka mshindi wa nafasi ya urais, serikali yake imekuwa ikishutumiwa sana kwa rushwa. Kumekuwa kukifanyika malipo mara dufu na mamilioni ya fedha yakipotea bila maelezo sahihi, ambapo kwa namna moja ama nyingine, watu wake wa karibu, mfano Makamu wake William Ruto, Mkewe Mama Margaret Kenyatta na Katibu wa Baraza la Mawaziri Bi Anna Waiguru wamekuwa wakihusishwa. Kutokana na picha hii inayoonekana kuwatia doa raia wa nchi hiyo, Maaskofu wanawaalika wakenya kujichunguza dhamiri na kujibu swali la: Je!, ni Kenya ya aina gani wanaitaka. Ni imani ya Maaskofu kwamba kila mwenye dhamiri safi anahitaji Kenya isiyo na rushwa, ghasia wala mmong’onyoko wa maadili, bali Kenya yenye amani na ustawi kimaendeleo.

Baraza la Maaskofu linatoa tahadhari kwamba, wakati wa kusimamisha wagombea kwenye hatua za vyama, kumeonekana tayari hatari ya kuwagawa raia wa Kenya na kuvuruga amani. Mwaliko wa kuzingati umoja wa taifa na kupiga vita ukabila, kupiga vita ujengaji wa chuki dhidi ya wagombea fulani, kukemea tabia ya uchaguzi unaohamasisha ghasia kutoka kwa wagombea na viongozi wa vyama na serikali, kukwepa wagombea wenye mwelekeo wa kuvuruga tunu msingi za familia na maisha ya urafiki. Maaskofu wanawaalika raia wote kuwachunguza vema wagombea kwa kuzingatia tabia zao katika ukweli, haki, uaminifu na maadili mema, kwani mafanikio na usalama wa familia za Kenya vitakuwa mikononi mwa watakaochaguliwa.

Tume huru ya Uchaguzi nchini Kenya isimamie wajibu wake na kuhakikisha inatembea kwenye kanuni za Katiba ya nchi, ambapo kuna usawa na uwiano wa uwakilishi kijinsia na wenye changamoto za ulemavu. Uchaguzi utakuwa wa haki, amani na wa kuaminika, iwapo taratibu zote zitazingatiwa. Misingi ya demokrasia, heshima kwa utu wa binadamu, na uhuru kwa kila mhimili wa utendaji vipewe kipaumbele kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wa kitume, Africae Munus, Dhamana ya Afrika, anafundisha kwamba uchaguzi ni ishara ya maamuzi ya raia na utawala halali, ambapo uhuru wa kuchangia mawazo au kujieleza unapoheshimiwa, hutia moyo ushiriki hai wa kila raia katika kujenga taifa lao (Rej., Afriace Munus, 81).

Vyama vya siasa ni kwa ajili ya kuhudumia raia, na sio kujitafutia maslahi binafsi. Ghasia baada ya uchaguzi wa 2007/2008 nchini Kenya, zilihamasihwa na viongozi wa vyama vya siasa, jambo ambalo ni kinyume kabisa kwa heshima na utu wa binadamu na ni kinyume cha utafutaji wa mafao ya wengi. Baraza la Maaskofu linasisitiza kwamba, linatambua kuwa kuna waamini wakatoliki kwenye kila chama cha siasa. Kanisa Katoliki halina upendeleo wowote wa chama au mgombea, isipokuwa linawaalika raia kujichunguza na kuwachunguza vema wagombea, kisha wafanye maamuzi kwa kufuata dhamiri zao. Katika yote, Maaskofu wanakemea sana rushwa zinazoshawishi wapiga kura kuchagua wagombea fulani na hivyo kuvunja misingi ya uadilifu. Baraza la Maaskofu nchini Kenya linasisitiza sana kwamba uchaguzi lazima uwe wa uhuru, haki na amani.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.