2017-06-24 17:23:00

Kanisa linawahitaji mashuhuda wa imani, maadili na utu wema!


Karibu ndugu msikilizaji katika kipindi cha tafakari ya Neno la Mungu, idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. Katika Domenika ya 12, mwaka A wa Kanisa, masomo yanatuelekeza kuwa watu wa kusimamia kweli na haki, hata katika mazingira ya kuonewa, kushutumiwa ama kushawishiwa sana, kwani kukubali kuanguka dhambini ni kukaribisha mauti. Karibu tutafune hili Neno kwa siku ya leo, liweze kutufaa katika uaminifu wa maisha yetu.

Ndugu msikilizaji, inawezekana umewahi kukutana na mazingira ambapo unazungukwa na vishawishi kiasi cha kudhani kana kwamba huna namna nyingine ila tu kujilegeza na kudondoka kwenye kishawishi hicho. Mara kadhaa unaweza kujitafutia hata visababu vya shida, mahitaji, ugumu wa maisha au kisingizio eti mbona fulani na fulani wanafanya au wanaishi kinamna hiyo, au kudhani ni sawa kwa kuwa watu hawakuoni au wengi hawatafahamu. Lakini utagundua kwamba ulipojiachia kwenye dhambi, matokeo yalikurudia kwa wakati wake, ukalionja joto la jiwe, kwani mshahara wa dhambi ni mauti (Rej. Warumi 6: 23).

Nabii Yeremia anasongwa na mashutumu mengi na watu ambao lengo lao ni kumfanya akate tamaa, ahadaike atende dhambi, apungukiwe kinga ya Mwenyezi Mungu waweze kumtenda vibaya zaidi (Rej. Yeremia 20:10). Hata hivyo nabii Yeremia anabaki kuwa mwaminifu akijua kwamba, Mwenyezi Mungu huichunguza mioyo ya wanadamu, anafahamu uadilifu wa kila mmoja, naye huwapigania walio wanyoofu (Rej. Yeremia 20:12). Mwanadamu unapojiachia kwenye anguko la dhambi kwa sababu zozote au visingizio vyovyote, unapungukiwa kinga ya Mwenyezi Mungu na kukaribisha mauti. Mauti hapa ieleweke kama kuharibikiwa kimaisha, ambapo mambo hayakuendei kama inavyopaswa, unakosa furaha na amani. Sio furaha au amani ya dunia, bali ile ya kweli. Maana Kristo anapokupa amani anasema: Nawaachieni amani, amani yangu nawapa. Siwapi ninyi amani kama vile ufanyavyo ulimwengu (Rej., Yohane 14:27).

Iwapo unajikuta katika hali ya dhambi ni muhimu kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho aliyotuachia Kristo. Hata hivyo Sakramenti hii sio kama bafu au bwawa, unajichafua unavyotaka na kwenda kuungama. Mwanadamu ni dhaifu, Mungu anaelewa hilo, ila kuna mambo ambayo mwanadamu unapoendekeza, huwezi kusingizia udhaifu tena, sababu unafanya makusudi ukiwa na akili timamu, jambo hili halimpendezi Mwenyezi Mungu. Mwanadamu unao uwezo wa kushinda vishwawishi sababu sheria ya dhambi iliyokuwa inatawala kabla, Kristo ameishinda kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake (Rej., Warumi 5: 14 – 15). Bwana asema: Tena kama mtu mwadilifu anauacha uadilifu wake na kutenda uovu, nami nikamwekea kikwazo, mtu huyo atakufa (Rej., Ezekieli 3:20).

Ndugu msikilizaji, Kristo anakualika usiogopeshwe na mtu wala kitu chochote kiasi cha kuhadaika ukatenda mabaya. Uwe jasiri na kubaki mwaminifu, hata unapowekewa vikwazo au vitisho, hata unapolazimika kutoa sadaka kubwa. Baki mwaminifu, kuwa mtu wa haki, kuwa mwema, kuwa mwadilifu muda wote sababu yote yafanyikayo sirini wakati hufika ambapo yatafunuliwa na kuwekwa wazi mbele ya watu (Rej., Mathayo 10:26), na hapo ndipo huwapo aibu ya siku unapoamua kutembea mtupu unakutana na wakwe.

Wala usidanganyike kwamba nimetenda dhambi lakini sijapatwa chochote. Mungu ana nyakati zake za kujibu (Rej., Sira 5:4). Wala usiidhihaki Sakramenti ya Kitubio kwa kusema Bwana ana huruma. Ni kweli Bwana ana huruma, lakini unapofanya makusudi, Bwana hafurahii. Kama inavyofundisha Hekima ya Yoshua mwana wa Sira: usiseme huruma yake ni kubwa, yeye atanisamehe dhambi zangu nyingi. Kumbuka Yeye ana huruma na ghadhabu, na hasira yake huwakumba wenye dhambi. Usichelewe kumrudia Bwana, wala usiahirishe siku hata siku. Maana ghadhabu ya Bwana itakuwakia ghafla, na wakati wa hukumu utaangamia (Rej., Sira 5: 6 -7). Bwana anaelewa kwamba dunia hii imejaa vishawishi vingi, ugumu wa maisha, vikwazo na vitisho vinavyoweza kumpelekea kuwa na hofu na kuanguka dhambini. Kwa sababu hiyo anakusisitiza utafakari kwa kina juu ya uzima wa roho yako na sio mambo ya kimwili yanayopita: msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu (Rej., Mathayo 10: 28).

Hitimisho:

Ndugu msikilizaji, ninapohitimsha tafakari ya leo, nikualike kudumu katika uaminifu wa maisha kwa kuzingatia uzima wa roho yako na sio tamaa za mambo ya dunia, kama anavyofundisha mtume Paulo: Fikra za mwili huleta kifo, fikra za roho huleta uhai na amani. Maana, mwenye kutawaliwa na fikra za mwili ni adui wa Mungu, haitii sheria ya Mungu, wala hawezi kuitii. Watu wanaotii matakwa ya mwili hawawezi kumpendeza Mungu (Rej., Warumi 8: 6-8). Ushindi wa vishawishi hutokana na moyo wa kutii sheria ya roho, sheria ya uaminifu na uchaji kwa Mungu, kwa maana kama asemavyo Kristo: roho ndiyo iletayo uzima, mwili hauwezi (Rej., Yohane 6:64).

Shukrani kwa Sr. Marximilliana Massawe na kwa niaba ya watangazaji wenza, nakushukuru kwa kuwa pamoja nasi leo, karibu tena kipindi kijacho. Kwa sauti ya kinabii, nakuaga nikisema.

Tumsifu Yesu Kristo

Laudetur Iesus Christus!

Padre Celestine Nyanda.








All the contents on this site are copyrighted ©.