2017-06-24 17:00:00

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Colombia: Ratiba elekezi


Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kutembelea nchini Colombia kuanzia tarehe 6 – 11 Septemba 2017 kama sehemu ya mchakato wa kuenzi maridhiano, haki na amani, baada ya Colombia kuwa katika mapigano kwa muda mrefu. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu ataondoka mjini Roma, Jumatano tarehe 6 Septemba 2017 na kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bogotà  saa 10:30 Jioni kwa saa za Ulaya na kupatiwa mapokezi ya kitaifa. 

Alhamisi, tarehe 7 Septemba 2017 akiwa mjini Bogotà atakutana na viongozi wa Serikali; atatembelea Kanisa kuu  la Jimbo kuu la Bogotà na kuwasalimia waamini watakaokuwepo katika eneo la Makao makuu ya Jimbo kuu la Bogotà. Baba Mtakatifu pia anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia na jioni kabla ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Uwanja wa Simon Bolivar, atakutana na kuzungumza na Kamati kuu ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM katika Makao makuu ya Ubalozi wa Vatican nchini Colombia.

Ijumaa, tarehe 8 Septemba 2017, Baba Mtakatifu atasafiri kuelekea Villavicencio na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu huko Catama. Majira ya jioni, kutafanyika Ibada ya Upatanisho wa kitaifa katika uwanja wa Las Malocas. Atapata nafasi ya kutafakari kwa kitambo mbele ya Msalaba wa Upatanisho wa Kitaifa na baadaye, atarejea tena mjini Bogotà. Jumamosi, tarehe 9 Septemba 2017, Baba Mtakatifu atatembelea mji wa Medellin na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Uwanja wa Ndege wa Enrique Olaya Herrera huko Medellin na baadaye atakutana na waamini na hatimaye, kabla ya kurejea tena mjini Bogotà, Baba Mtakatifu Francisko atakutana na kuzungumza na wakleri, watawa pamoja na familia zao kwenye Uwanja wa Macarena.

Jumapili, tarehe 10 Septemba 2017, Baba Mtakatifu ataondoka na kuelekea Cartagena. Huko anatarajiwa kubariki jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kwa ajili ya watu wasiokuwa na makazi. Huu ni mradi unaofadhiliwa na Kikundi cha Talitha Qum. Tukio hili litafanyika kwenye Uwanja wa Mtakatifu Francisko wa Assisi pamoja na kusali Sala ya Malaika wa Bwana pamoja na waamini watakaokuwepo. Baba Mtakatifu atatembelea Madhabahu ya Mtakatifu Petro Claver na baadaye ataadhimisha Ibada ya Misa takatifu katika eneo la Bandari ya Contercar. Baada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko atakuwa anakunja vilago vya hija yake ya kitume nchini Colombia kwa Mwaka 2017, tayari kurejea tena mjini Vatican. Anatarajiwa kuwasili mjini Roma, Jumatatu, tarehe 11 Septemba 2017 majira ya mchana. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakuwa nawe bega kwa bega ili kukujuza yale yanayojiri wakati wa hija hii ya upatanisho nchini Colombia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.