2017-06-23 14:37:00

Wakumbukwa wahamiaji waliofariki katika safari ya matumaini


Kulinda na kutunza uhai wa binadamu ni wajibu wa kila mmoja. Ni wajibu kiutu, kidini, kimaadili na kijamii. Haiwezekani kuhudumia na kuhangaikia wahanga wa majanga yanayomkumba mwanadamu leo bila kusutwa na dhamiri, bila kupambana kupiga vita vifo vya wanyonge, bila ukarimu uliojaa upendo. Hii ni sehemu ya mahubiri ya Padre Marco Gnavi, Paroko wa Kanisa kuu la Mt. Maria la Trastevere, wakati wa Misa Takatifu ya mkesha wa sala, siku ya Alhamisi, tarehe 22 Juni 2017, mkesha ulioandaliwa na Jumuiya ya Mt. Egidio kwa ajili ya kuwaombea marehemu wahamiaji waliopoteza maisha yao wakati wa safari ya matumaini, wakikimbia nchi zao kutoka Bara la Afrika, Asia na Mashariki ya kati, ili kutafuta hifadhi nchi za Ulaya.

Kristo alitabiri juu ya ishara za nyakati za mwisho ambapo taifa litanyanyuka kupigana na taifa lingine, matetemeko ya ardhi, njaa, magonjwa, majanga, vituko na ishara za kutisha kutoka angani (Rej., Luka 21: 11). Katika nyakati kama hizi ambapo dunia inashuhudia mambo haya, ni muhimu binadamu kushikamana kwa ukarimu ili kusaidiana kwa ajili ya wokovu wa wote. Padre Gnavi anawaalika waamini wasichoke kuwahudumia na kuwahangaikia wahamiaji, kwani atakeyevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka.

Wokovu ni uhalisia unaounganisha waamini na sio kuwatawanya au kuwatenganisha. Katika hali ya mahangaiko mengi katika jamii za leo, ni mwaliko wa kushikamana kidugu na kwa upendo. Waamini wasiingiwe hofu ya kupungikiwa, hofu ya mipaka, hofu ya utaifa, lugha, tamaduni, au uchumi, kwani hili litawadhoofisha na kuwaangusha kiimani. Waamini wadumu katika uaminifu wa Injili, wakiwa na matumaini na kumtegemea Kristo, kwani ni yeye mwenyewe ameahidi katika mahangaiko kama hayo: mimi mwenyewe ntawapeni ufasaha wa maneno na hekima (Rej., Luka 21:15).

Wakati wa mkesha huo wa sala kuwaombea marehemu wahamiaji waliofariki wakati wa safari ya matumaini kuelekea Bara la Ulaya, yamesomwa majina na historia za wahanga hao, ikiwa ni ishara ya matumaini ya uhakika ambayo Bwana anawahakikishia waje wake kwamba wana thamani kubwa machoni mwa Baba wa mbinguni, maana hata nywele za vichwa vyao zimehesabiwa zote, hivyo mbele ya Mungu, hawatapotea kamwe (Rej., Luka 12:7).

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.