2017-06-23 16:06:00

Papa: Urafiki wa kweli unagusa undani wa mtu, ni faraja na upendo!


Makubaliano ya “Serra International” ni Shirika la Waamini Walei linalojihusisha katika mchakato wa kutegemeza miito ya kipadre na kitawa ndani ya Kanisa. Kuanzia tarehe 22- 25 Juni 2017 linaadhimisha mkutano wake wa 75 unaongozwa na kauli mbiu “Siempre Adelante. Il coraggio della vocazione” yaani “Mbele daima, ujasiri wa wito”. Hii ni changamoto kwa waamini walei kushiriki kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, kila mwamini kadiri ya karama na mapaji aliyokirimiwa na Roho Mtakatifu. Ni watu wanaowafariji jirani zao kwa mafuta ya huruma ya Mungu na kwamba, imani inawawezesha waamini kuwa ni marafiki!

Kwa njia hii, waamini walei wanajitaabisha usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, wanawasaidia wakleri na watawa katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa, kielelezo cha utajiri mkubwa katika Kanisa. Mwanashirika wa Serra ni mwandani wa padre au jandokasisi ambaye Mwenyezi Mungu amemwekea pembeni mwake, kiasi cha kuwa ni jirani na rafiki wa kweli mintarafu mzizi neno na wala si kama linavyotumika katika ulimwengu wa digitali. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 23 Juni 2017 kwa kumshukuru Dr. Dante Vannini, Rais wa Makubaliano ya “Serra International” alipokutana na kuzungumza nao, mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, urafiki wa kweli unamgusa mtu mzima kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza, kama alivyofanya Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba na akawaita wafuasi wake kuwa ni rafiki zake, kwani aliwafunulia siri zote za mbinguni, ili kujenga uhusiano mwema kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu mdhambi. Huu ni uhusiano unaovuka mipaka ya sheria kwa kujikita katika fadhila ya upendo usiokuwa na mipaka. Huu ni urafiki unaowajibisha, kiasi cha kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Urafiki wa namna kama hii unagusa undani wa maisha ya watu husika kwa kufumbata: huruma, faraja, mshikamano; ukweli na uwazi, nyenzo msingi za kumwinua na kumsimamisha, rafiki aliyeteleza na kuanguka.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, huu ndio urafiki ambao Makubaliano ya “Serra International” unataka kujenga na kuwamegea pia wakleri: kwa kuwasindikiza katika imani; uaminifu katika sala na dhamana ya utume wao; watu wanaoshirikishana ladha ya wito wa Kikristo; kwa kuwa na ujasiri wa kufanya maamuzi makini; kwa kuonesha furaha na uchovu wa kitume. Hawa ni marafiki wanaotambua umuhimu wa kuwa karibu na wakleri, kwa kuwaangalia kwa wema na uelewa; kwa ukarimu na upole katika udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu. Wao wanakuwa ni mahali pa faraja kama ilivyokuwa kwa familia ya Maria na Martha kwa Yesu mwenyewe.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, wito wa Kikristo ni mwaliko wa kusonga mbele daima, kurudi nyuma ni mwiko! Ni hija takatifu inayowataka waamini kuacha nchi yao wenyewe, usalama wa maisha yao na kuanza kuelekea katika nchi ya ahadi, ili kukutana na ndugu zao katika Kristo Yesu. Wito ni mwaliko wa kutoka katika undani wa mtu binafsi ili kuanza kuishi ile furaha ya kukutana na Kristo Yesu, tayari kumfuata katika njia ile anayowaonesha. Hii ni hija inayofanywa katika majadiliano na ujasiri wa kujisadaka pasi na kujibakiza; tayari kupambana na mawimbi mazito ya bahari, ili kukumbatia upendo wa Mungu. Mapadre wanapaswa kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa huduma ya Injili.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao, huku wakithubutu kuonesha kipaji chao cha ubunifu; kwa kukumbatia changamoto zinazoletwa mbele yao kwa njia ya Roho Mtakatifu, hata pale inapowabidi kubadili mwelekeo wa maisha na miundo mbinu iliyoko mbele yao! Hivi ndivyo alivyoshuhudia Mtakatifu Junipero alipoanza safari yake kuelekea San Diego, ili kupandikiza Msalaba, yaani Injili ya Kristo! Ni hatari sana kwa Wakristo wasiothubutu kutembea, waamini wanaojifungia katika ubinafsi wao, hawa kwa hakika wanakuwa ni sehemu ya “Wakristo wa Makumbusho”; wanaoogopa kufanya mageuzi katika maisha; wanaoshindwa kutumia karama na mapaji yao kwa ajili ya huduma ya Injili, bali wanajilinda wao wenyewe na mafao binafsi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wito ni mwaliko wa kutoka katika undani wa mtu mwenyewe tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma na mradi mkubwa. Kwa njia ya unyenyekevu, waamini wanakuwa ni watenda kazi katika shamba la Bwana, kwa kukataa umaarufu na majigambo yasiyokuwa na tija wala mvuto! Viongozi wa Kanisa wawe na ujasiri wa kuwaachia wengine kuendeleza kazi na wajibu wao bila woga wala wasi wasi. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwashukuru wajumbe wa Makubaliano ya “Serra International” kwa upendo na majitoleo yao ya kusaidia kuhamasisha miito kwa njia ya sala na ushiriki wao katika shughuli za kitume. Anawataka kusonga mbele daima katika matumaini, utume kwa kuwa na mwono mpana zaidi unaowashirikisha hata vijana wa kizazi kipya, ili kuweza kuwaandalia leo na kesho iliyo bora zaidi. Kanisa na wito wa Kipadre, unawahitaji sana. Bikira maria, Mama wa Kanisa na Mama wa Mapadre awasindikize katika maisha na utume wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.