2017-06-23 16:26:00

Papa Francisko: Jifunzeni upole na unyenyekevu kutoka kwa Kristo Yesu


Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma, neema, mapendo na baraka kwa waja wake. Hii ni siku iliyotengwa na Mama Kanisa ili kuwakumbuka na kuwaombea Mapadre katika maisha na wito wao, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa. Ili kuweza kutekeleza vyema dhamana na utume huu, kuna haja kwa Mapadre kujifunza kuwa na moyo wa unyenyekevu, upole na uvumilivu, kwa kutambua kwamba, wametwaliwa kati ya watu kwa ajili ya watu katika mambo matakatifu.

Wamekirimiwa upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mwana wake wa pekee! Wao wamechaguliwa kutoka miongoni mwa watu wa mataifa, ili kuweza kuadhimisha Mafumbo ya Ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 23 Juni 2017, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Mapadre wameteuliwa kwanza kabisa kwa njia ya huruma na upendo wa Mungu, kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu ameamua kuwa “mfungwa katika maisha ya watu wake”.

Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu ameamua kuambatana na binadamu katika hija ya maisha yao, kiasi cha kuendelea kuwa mwaminifu katika ahadi zake, huku akiwaonesha upendo na huruma yake isiyokuwa na kifani! Huu ndio ujumbe na kiini cha Habari Njema ya Wokovu, kinyume cha hapa ni kushindwa kutambua ukweli huu wa imani! Mwenyezi Mungu amependezwa na unyenyekevu wa watu wake, kiasi cha kuwateuwa kama vile Kristo Yesu alivyojifunua kwa watoto wadogo, akawaficha mambo haya watu wenye akili na hekima, kwani ndivyo ilivyompendeza Mwenyezi Mungu.

Yesu ameonesha unyenyekevu huu kwa kujitwalia hali ya ubinadamu katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi! Anawaalika wale wote wanaoteseka na kuelemewa na mizigo, waende kwake ili aweze kuwapatia pumziko la nguvu, kwani nira yake ni laini na mzigo wake ni mwepesi. Yesu anawachagua wanyenyekevu wa moyo kwani hawa wanaweza kuisikiliza sauti yake na kuifuata, lakini wenye akili na nguvu, inawawia vigumu kutokana na kujiamini kupita kiasi. Yesu amejinyenyekeza hata kifo cha Msalaba, ili kushuhudia utukufu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa mkuki ubavuni, humo yametoka maji na damu, alama na chemchemi ya Sakramenti za Kanisa! Huu ndiyo moyo unaopenda, unaochagua na kuendelea kuwa aminifu; kwa kushikamana na binadamu katika udogo na unyonge wake. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwamini Mwenyezi Mungu na Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo, kiini cha Fumbo na Imani ya Kanisa. Hii ni changamoto ya kuendelea kujinyenyekesha kwa kutambua kwamba, kwa njia ya fadhila hii ya unyenyekevu, Kristo Yesu, ameweza kuwakomboa wanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni changamoto ya kuadhimisha matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu; ni fursa ya kuadhimisha kazi ya ukombozi iliyotekelezwa na Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, kielelezo cha ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.