2017-06-23 08:52:00

Mwenyeheri Teofilius Matulionis alimshuhudia Kristo kwa kumwaga damu!


Tarehe 25 Juni 2017 huko Vilnius Lithuania, atatangazwa Mwenyeheri Askofu mkuu Teofilius Matulionis. Alizaliwa mnamo tarehe 22 Juni 1873 na akaanza majiundo yake ya ukasisi mnamo mwaka 1892 katika Seminari ya St. Petersburg huko Urusi, na mnamo tarehe 7 Marchi 1900 akapata Daraja Takatifu ya Upadre. Mnamo mwaka 1943 akawekwa wakfu kuwa Askofu wa Kaigiadorys, na kisha mnamo Februari 1962 akawa Askofu mkuu wa jimbo hilo hilo. Haukupita muda mrefu, mnamo tarehe 20 Agosti 1962 akafariki dunia akiwa na umri wa miaka 89.

Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, katika mahojiano na Radio Vatican anaelezea kwamba, kifo cha Askofu mkuu Teofilius Matulionis kilitokana na mateso ya gerezani. Kilikuwa ni kipindi cha nyanyaso kutoka kwa utawala wa Kinazi na wa Kikomunisti, lakini Askofu mkuu Teofilius Matulionis hakukatishwa tamaa kwenye utume wake, na alipambana kupinga chuki dhidi ya Injili ya Kristo na Kanisa lake, hata akaifia dini.

Jamii ya leo ina mazoea sana ya kutumia neno mfiadini au kuifia dini katika mazingira ambayo siyo sahihi sababu neno hili lina utamaduni wa muda mrefu na maana yakinifu katika maisha ya wakristo. Kardinali Angelo Amato anasema, kuifia dini ni kumfuasa Kristo unyayo kwa unyayo katika hija ya maisha, kwa mfano ule ule wa Kristo mwenyewe kuwa mnyenyekevu, mtii, bila hila wala mizigo ya dhambi, bali kwa uaminifu na moyo mkunjufu mpaka mauti ya msalaba. Katika hija ya maisha ambapo mwamini anauchuchumilia utakatifu hata mbele ya mauti, Kristo huwa ndani ya mwamini huyo akimtia nguvu na ujasiri. Wafiadini wanalifahamu vizuri Neno la Bwana anaposema: msiwaogope wale wanaoua mwili lakini hawawezi kuiua roho… Yeyote atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni (Rej., Mathayo 10: 28;32)

Askofu mkuu Teofilius Matulionis alipata mateso kwa miaka mingi sana chini ya utawala wa kinazi na wa kikomunisti uliopania kulitokomeza Kanisa. Seminari zilifutwa, mashirika ya kitawa ya kike na kiume yakatawanywa, Kanisa nchini Lithuania likazuiwa kufanya mawasiliano yeyote na makao makuu Roma, na kuzuiwa kila aina ya uchapishaji wa maandishi ya kikatoliki. Kanisa likaishi katika ukimya kama ukimya wa kaburi. Hata hivyo kama inavyofahamika, ni katika ukimya huo wa kaburi, ndipo inapatikana tafakari ya kutosha juu ya uhalisia wa maisha ya mwanadamu na ukuu wa Mwenyezi Mungu. Ndivyo ilivyo siku zote katika Kanisa waamini wanaponyanyaswa na Kanisa kuonekana kuwa ndani ya ukimya, ukuu wa Mungu hujidhihirisha zaidi.

Askofu mkuu Teofilius Matulionis akiwa katika kambi za kinazi aliendelea kuishi kipadri kwa tabia na mwenendo, akiwa mtulivu na kutegemea mapenzi ya Mungu, kiasi cha kuwavutia watu kumtambua kuwa kweli mtu wa Mungu na mtakatifu. Mwenendo wake huo uliwagusa hata watesi wake katika kambi hizo. Kwani baada ya kifo chake, Kamanda wa jeshi la kirusi alisema wazi “alikuwa mwanaume kweli kweli”. Zaidi watesi hao hao baada ya habari za kifo chake walianza kuhisi uwezekano kwamba siku moja Vatican itamtangaza mtakatifu na kaburi lake litakuwa sehemu ya kutembelea mahujaji. Yanayoelekea kutokea Juni 25, 2017 kwa namna fulani laweza kuwa  ni uthibitisho wa mithali: lisemwalo lipo, kama halipo linakuja.

Hili linatokana na ukweli pia kwamba, pamoja na mateso yote aliyopata kutoka kwa askari, hakuwahi kuwachukia wala kuwa na kinyongo. Siku zote Askofu Teofilius Matulionis alikuwa anatafuta mapenzi ya Mungu kati ya watu, hata wale waliokuwa wanatenda mabaya. Ndio kusema, hakujikita kwenye ubaya wa mtu, bali kwenye heshima na utu wa mtu huyo, kwa sababu kaumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hili ni fundisho hata leo, kutolipa baya kwa baya, kutochukia watu hata maadui, bali kuwapenda na kuwaombea, kinyume na hapo itakuwa kuisaliti damu ya wafiadini.  Kardinali Angelo Amato anasema, huu ni mwaliko kwa waamini wote kuishi maisha ya sala, kukumbatia mateso na kutenda kazi kwa ajili ya utukufu wa Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya wokovu wa roho za watu. Kusiwe na kuta za utengano ndani ya mioyo ya waamini, bali wajazwe roho ya ukarimu, utulivu, utu wema na huruma.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.