2017-06-23 13:40:00

Kard. Stella, mapadri wajenge urafiki na Kristo


Sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni siku pia ya kuombea utakatifu wa mapadri. Ni siku ya umoja, udugu na sala kati ya mapadri katika kuvumbua zaidi zawadi ya ukasisi ambao padre anaipokea bure kutoka kwa Kristo. Sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa mwaka huu, inaadhimishwa na Mama Kanisa, siku chache baada ya Baba Mtakatifu Francisko kufanya hija ya kitume maeneo ya Bozzolo na Barbiana, Italia, kwa heshima ya kumbukumbu ya mapadri Primo Mazzolari na Lorenzo Milani. Mapadri walioishi na kutoa huduma katika kweli, haki, uwazi, ujasiri, imani thabiti, ukarimu, huruma na wakijipambanua hasa katika kujali maskini na wenye kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, katika mahojiano na gazeti la Osservatore Romano, anachambua maana na umuhimu wa Sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa maisha na utume wa padre. Hii ni siku ya fursa kwa ajili ya sala na tafakari hasa katika nyanja tatu: kwanza ni umuhimu wa sala kwa maisha na utume wa padre, umoja na udugu kati ya wakleri na utafiti wa dhamiri na tathimini ya wito wao.

Maisha ya sala kwa padre ni ya msingi sana, ili kuepuka hatari ya kutenda kazi nyingi bila matunda yanayodumu. Utume wa padre ili ulete matunda ya kudumu ni lazima awe na mahusiano ya karibu na ya moja kwa moja na Kristo, hasa katika maisha ya sala. Kristo mwenyewe anasema: kama vile tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipobaki katika mzabibu, hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu (Rej., Yohane 15:4). Baba Mtakatifu Francisko anawaalika mapadri kuwa makini katika utume wao, wasijewakaishia kuwa kama maafisa wa umma katika mambo matakatifu. Waamini hawahitaji maafisa katika shamba la Bwana, wanahitaji wachungaji wema, wachungaji wa roho zao, wenye uwezo wa kusikiliza, kuwakirimu, na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao. Hili linawezekana kwa mapadri wanaodumu katika maisha ya sala.

Mapadri wanapaswa kuishi katika umoja na udugu pamoja na wakleri wenzao wakishikamana na Askofu wao aliye ishara ya umoja na udugu kati yao. Maisha ya upweke pweke na kujitenga yanahatarisha anguko la wakleri. Hatari ya jeshi la mtu mmoja katika mapambano dhidi ya utawala wa shetani, ni kuanguka anguko la mende, miguu juu unabaki unafurukuta kimgongo mgongo bila msaada. Udugu huu unapaswa uwe udugu wa kweli na sio unafiki wa mdomoni. Wakleri waoneshe uzuri wa udugu kati yao, ili kufanya utakatifu wa maisha na utume wao ung’are kwa kusaidiana na kutembea pamoja, ndipo Baba wa mbinguni hutukuzwa kupitia wao.

Mapadri wajitathimini na kuvumbua tena kiini cha wito wao, utambulisho wao na huduma yao kati ya Taifa la wana wa Mungu. Wito wa padre ni zawadi ambayo Kristo anamkirimia padre sio kwa sababu ni mkamilifu au kwa sababu ana vipaji vya pekee sana, bali kwa sababu anawashirikisha pendo lake la kimungu ili wao pia wawashirikishe pendo hilo hilo wale wanaowahudumia. Kristo anawaita watu kama wavuvi na watoza ushuru. Watu ambao hawana elimu kubwa ya kutisha au vipaji vya pekee sana. Katika unyonge na udhaifu wao, Kristo ndiye anayewafundisha nini cha kufanya, na namna gani ya kuwa kama asemavyo kwa wanafunzi wa kwanza: nifuateni, nami nitawafanya ninyi kuwa wavuvi wa watu (Rej., Mathayo 4:19). Padre hajifanyi kuwa mvuvi wa watu, bali ni Kristo ndiye anayemfanya mvuvi na kumfunza namna ya kutimiza utume huo.   

Kuwa wadhaifu na kuwa wavuvi wa watu ni uhalisia wa mapadri ambao unategemeana sana kwa pamoja na haswa ndio uhakika wa kuchuchumilia utakatifu, vinginevyo wangalikuwa wakamilifu, mapadri wangalijisahau, wakajivuna na kumpotezea Mungu ambaye ndiye haswaa anayewatuma. Kumbe katika maisha na utume wao, mapadri katika unyonge na udhaifu wao wanapaswa kuuchuchumilia utakatifu wakiitegemea sana huruma na neema ya Mungu. Kama vile mtume Paulo anavyoshuhudia hilo: nilimsihi Bwana mara tatu kuhusu jambo hili ili linitoke. Lakini akaniambia, neema yangu inatosha kwa ajili yako, maana uwezo wangu hukamilishwa zaidi katika udhaifu (Rej., IIWakorintho 12:8-9).

Baba Mtakatifu Francisko anawatahadharisha mapadri kutokuwa wanafiki na kujipamba ili kujionesha kana kwamba ni vyombo vya dhahabu, la hasha!, wajitambue na kujidhihirisha kama vyombo vya udongo, ambavyo katika udhaifu huo, wanairuhusu neema ya Mungu iwafinyange na kuwaunda kuwa nyenzo za utumishi anaoutaka Mungu Mwenyewe.

Kardinali Beniamino Stella anasema, padre anapaswa kuwa mchungaji kati ya watu, pamoja na watu, akishiriki maisha yao ya kila siku, akiguswa na madonda ya mahangaiko yao ya maisha, kisha anawaganga kwa mafuta ya Furaha ya Injili. Padre ni daraja kati ya Mungu na watu, hivyo hana hofu ya kutojichafua kwa kuwahudumia kondoo wa Bwana, bali anajishughulisha kikamilifu na kubaki na harufu ya kondoo hao, kwani anakuwa sehemu kweli ya maisha yao.

Ili kweli padre aweze kuwa mchungaji wa namna ambayo Kristo anamhitaji, inabidi aandaliwe vizuri. Kwa sababu hiyo, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri linasisitiza majiundo bora ya majandokasisi katika seminari. Kardinali Beniamino Stella anasema, ni lazima walezi waandaliwe vizuri, na wawe na uwezo wa kutoa malezi na mfano bora kwa majandokasisi, ili waseminari hao waweze kukua na kukomaa kiimani, kisaikolojia, kimahusiano, kielimu, kichungaji na kiroho.

Maisha na utume wa padre utakuwa na mabonde na milima. Uhalisia wa maisha ya mwanadamu, padre hawezi kuukwepa kwani hakuna kinga katika hilo. Jamii ya leo inazo changamoto na matatizo mengi. Zipo sehemu zenye hali ngumu sana ya umaskini, vita, matabaka, ukosefu wa haki na usawa, na kinzani mbali mbali ambapo kuna nyakati inaonekana kuwa ngumu kushuhudia imani na zaidi sana kuishi vema utume wa kipadre.

Kardinali Beniamino Stella anasema, kwenye hali kama hizo, padre asichoke wala kukata tamaa, bali washikamane kwa pamoja katika udugu wa kipadri, na kila mmoja azidi kujenga mahusiano binafsi na Kristo katika sala. Changamoto katika utume huwakomaza mapadri, kwani ni wakati wa kutafuta njia mpya za uinjilishaji, ili Neno la Bwana lizidi kupenyeza katika kuleta wokovu kwa roho za watu, ikiwa ni ushuhuda kwamba, Neno la Mungu halishindwi wala halikwamishwi na chochote.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.