Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Jengeni utamaduni wa Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu!

Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya huruma, upendo na msamaha wa kweli! Changamoto ni kuendelea kuwahamasisha waamini kujenga utamaduni wa Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. - ANSA

23/06/2017 16:57

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu imetengwa na Mama Kanisa kwa ajili ya kuombea wongofu na utakatifu wa maisha na wito wa Kipadre kwani kimsingi Mapadre ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Hivyo basi, wanapaswa kupenda na kuhurumia kama ambavyo Kristo mwenyewe anavyowahurumia watu wake. Padre Wojciech Adam Koscielniak, Paroko wa Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu ni sehemu ya vinasaba vya maisha na wito wake wa Kipadre.

Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake na kwamba, upendo huu unamwilishwa kwa namna ya pekee katika maisha na utume wa Mapadre, ambao kimsingi ni Makuhani wa Agano Jipya na la Milele. Wanapaswa kumjifunza Kristo Yesu ambaye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo. Kwa njia ya Mapadre, wema, upole na utakatifu wa maisha unaweza kuwafikia waamini mahali waliko. Moyo wa Yesu uliotobolewa kwa mkuki ukabaki wazi, humo ikatoka damu na maji, alama za Sakramenti za Kanisa, yaani Sakramenti ya Ubatizo na Ekarististi takatifu; uwe ni ukumbusho kwa Mapadre kwamba, hata wao katika maisha na utume wao, wanaweza kuchomwa na mikuki ya maneno n ahata wakati mwingine kuanguka katika udhaifu wao wa mwili, lakini bado wanakumbushwa kwamba wao ni chemchemi ya huruma, upendo na msamaha kwa ajili ya watu wa Mungu. Kumbe, Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa familia ya Mungu mahali walipo! 

Padre Wojciech Adam Koscielniak, Paroko wa Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, anapenda kuchukua nafasi hii kuwaalika waamini kujenga utamaduni wa Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kutimiza masharti yote yanayotolewa, ili kujipatia rehema na neema zinazotolewa na Kristo Mwenyewe kwani daima ni mwaminifu kwa ahadi zake. Watoto wanaopokea Sakramenti za Kanisa wajengewe utamaduni wa Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu kama inavyojionesha katika ushuhuda wa maisha yake mwenyewe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

23/06/2017 16:57