2017-06-23 10:08:00

Iweni ni mashuhuda na wajenzi wa Ufalme wa Mungu kwa matendo zaidi!


Ndugu zangu, karibuni katika tafakari yetu dominika hii ya leo. Dhamira inayotuongoza ni habari ya ufalme wa mbingu.Maisha ya hadharani ya Yesu katika injili ya Matayo yanatanguliwa na hotuba kuu tano na kila moja ikitanguliwa na shughuli mbalimbali za Bwana ikiwepo miujiza. Lengo kuu likiwa ni kuweka wazi vipengele vya ufalme wa Mungu, ambalo ndilo lilikuwa jukumu la kwanza la Bwana.  Kwa kifupi ufalme huu wa Mungu ni ufalme wa upendo na amani na usiotawaliwa na aina yo yote ile ya dhambi. Katika Agano Jipya, ufalme wa Mungu unaonekana katika ukamilifu wake siku za mwisho. Hii inajidhihirisha pale Yesu anaposema katika Marko 1:15 – akisema, wakati umefika, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini injili. Hapa Bwana Yesu alimaanisha habari ya ule ukamilifu ulio katika ufunuo wa Mungu Baba.

Wakristo wa kwanza, baada ya ufufuko wa Yesu, walitambua kwamba ufalme umekaribia katika Kristo  mwenyewe na katika ujumbe wake. Hata hivyo walikwazwa na kutokuamini kwa watu wote na hivyo ikabidi wawekeze matumaini yao katika ujio wa pili wa Kristo.  Lakini katika kipindi kati ya ufunuo wa kwanza na ule wa pili, mambo mengi yalitakiwa kufanyika. Yesu alisia mbegu na wafanyakazi walihitajika. Ule ujumbe wa ufalme wa Mungu uliotangazwa na Kristo, ulitakiwa uenezwe kwa ulimwengu mzima.

Mwinjili Mathayo anaona hili likifanywa na kanisa na amepanga hizo hotuba tano kwa namna ambayo unaonekana uhusiano wa wazi kati ya ufalme wa Mungu na uenezwaji wake ukifanywa na kanisa. Kwa mfano katika hotuba ya kwanza –  hotuba ya mlimani – tunapata mwongozo mzima wa namna ya kuupata ufalme wa Mungu, namna ya kuupata ufalme katika kanisa. Kanisa lina wajibu wa kuutangaza ufalme huo. Masomo yetu ya leo ni sehemu ya hotuba ya pili. Ni hotuba ya kimisionari ikihusisha utume wa wale 12 na jinsi ya kuenenda huku wakieneza habari za ufalme. Huu ndo umekuwa mwenendo wa utendaji wa wamisionari kwa karne nyingi.

Kwa namna ya pekee katika Injili tunasikia habari juu ya mateso na jinsi ya kusema au kujibu. Wanaagizwa wasiwe na woga na wawekeze pamoja na Bwana wao.  Ingawa miongozo hii imewekwa wazi kwa ajili ya wale ambao kwa namna ya pekee hutambulika kama wamisionari, ieleweke wazi kuwa ni wajibu wa kila mkristo na mfuasi. Na ujumbe huu unatukumbusa kuwa ujumbe wa ufalme ni kama bomu ambalo hutoa tishio. Upinzani utakuwepo, ni ujumbe ambao ukieleweka unaweza kupokeleka au kupingwa. Bwana anatualika tuongee wazi wazi na bila woga tena hadharani. Yesu alifanya na kutimiza wajibu wake kwa wakati wake. Wafuasi wake ndio sauti yake ulimwenguni kote.  Pamoja na hatari zo zote zile, matumaini yetu na uhakika wetu haupo katika kukubalika katika msimamo wetu, kama Yeremia katika somo la kwanza, lakini tu katika Bwana. Yeye analinda watu wake. Huu ndio uhakika wa huo ufalme. Ndiyo unaofanya umisionari uwezekane.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.