2017-06-23 14:21:00

Askofu mkuu Auza, Utawala wa sheria unalinda na kutetea uhai


Utawala wa sheria unajihusisha sana kwenye kulinda na kutetea haki msingi za binadamu. Wanadamu wote wana thamani na utu usawa. Kwa sababu hiyo haki ya kuishi inapaswa kutetewa kwa watu wote na kwa muda wote wa maisha bila kubagua hali, majira wala nyakati. Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, akitoa Hotuba yake kwenye Mkutano mkuu wa Umoja wa Nchi za Amerika mjini Cancun, nchini Mexico hivi karibuni, amewaalika nchi wanachama wa Umoja huo kuitazama upya haki ya kuishi kwa watoto wachanga, wahamiaji, maskini, wenye changamoto ya ulemavu, wazee na wanaohukumiwa adhabu ya kifo.

Umoja wa Nchi za Amerika ulianzishwa mnamo mwaka 1948, ukiwa na nchi wanachama 35, kwa lengo la kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Tangu tarehe 19 – 21 Juni 2017, Umoja huo umekuwa na mkutano mjini Cancun kwa nia ya kutafuta muafaka wa hali tete ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini Venezuela.

Askofu mkuu Bernadirto Auza anasema, Vatican inazidi kuwatia moyo Umoja wa Nchi za Amerika waongeze nguvu katika kutetea haki msingi za binadamu. Nguzo za maendeleo endelevu ya binadamu kama vile malazi, ajira, mshahara stahiki, chakula, maji safi na salama, uhuru na maisha ya kiroho vinapata msingi wake kwenye haki ya kuishi. Ujumbe wa Vatican unasikitishwa na hali za wanaoshikiliwa na vyombo vya dola na usalama bila taratibu za kisheria, wanaoshitakiwa na kuonewa bila makosa, wenye changamoto ya afya ya akili na kwa wengi ambao hawana wakili wala rasilimali za kupigania haki zao. Ujumbe wa Vatican unaalika juhudi zifanyike ili haki za watu hawa ziweze kutambulika na kulindwa kisheria.

Utawala wa sheria na uhuru wa kujieleza vina mahusiano ya karibu sana. Hivyo inaposikika mauaji ya waandishi wa habari, wachunguzi wa mambo na wateteaji haki, ni ishara ya wenye nguvu kutaka kukwepa uwajibikaji kisheria. Suala hili ni kinyume kabisa na haki za binadamu, na ni sumu mbaya inayoangamiza demokrasia ndani ya utawala wa sheria.

Askofu mkuu Auza anasema, uhuru wa kujitegemea kwa mhimili wa mahakama ni sehemu msingi ya uatwala wa sheria na kwa upatikanaji wa haki kwa kila mtu katika jamii husika. Hivyo kama Baba Mtakatifu Francisko anavyosema, mhimili wa mahakama unapokuwa umeoza kwa rushwa, utawala wa sheria unaangukia mikononi mwa wenye nguvu na hivyo wanyonge wanaishia kuonewa. Ni mwaliko kusimamia haki katika kweli na uhuru, ili kila mmoja apate kilicho chake.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.