2017-06-22 07:17:00

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Siku ya kutakatifuza Mapadre


Leo tunaadhimisha sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Moyo ni ishara ya huruma na mapendo na hivyo tunapoadhimisha sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu tunaukumbuka upendo wake mkuu kwetu, kwa kujitoa kwake hata kufa msalabani kwa ajili ya wokovu wetu. Sala ya mwanzo ya sherehe hii inautambua Moyo huu Mtakatifu kama Moyo uliojeruhiwa kwa ajili ya dhambi zetu.Hivyo Moyo Mtakatifu wa Yesu ni ufunuo wa upendo wa Mungu kwetu. Upendo huu ndiyo unaolizaa Kanisa kwani ulipochomwa pale juu msalabani ilitoka damu na maji kama chemchemi ya neema. Tunachota katika chemchemi  hiyo Baraka zote za mbinguni kwa njia ya huduma ya Kanisa katika Sakramenti na Neno la Mungu.

Upendo wa Mungu kwetu ni mkubwa mno. Upendo huu unatujia si kwa mastahili yetu. Kitabu cha Kumbukumbu ya Torati kinaufafanua upendo huo kwa tendo la Mwenyezi Mungu kuwachagua Waisraeli. Waisraeli walichaguliwa na Mungu si kwa sababu walistahili bali kwa sababu Mungu ndiye aliwapenda. “Bwana hakuwapenda Ninyi, wala hakuwachagua ninyi kwa sababu mlikuwa wengi kuliko mataifa yote… bali kwa sababu Bwana anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia Baba zenu.” Matendo makuu ya Mungu kwa Waisraeli hayakusababishwa na ukubwa wao au weledi wao au utakatifu wao. La hasha! Ni upendo mkuu wa Mungu ambaye kwa upendo huo aliwaahidi kuwa nao na kuwalinda; aliahidi kuwakomboa kutoka maadui zao na kuwalinda.

Kristo ni utimilifu wa upendo huo. Mtume Yohane anatuambia kwamba: “si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba Yeye alitupenda sisi, akamtuma mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu”. Fumbo la umwilisho linaukutanisha umungu na ubinadamu. Kwa kuutwaa ubinadamu wetu Kristo anaishi katika hali zote za kibinadamu isipokuwa dhambi na mwishoni anamkomboa mwanadamu na dhambi. Mwanadamu muhasi anahangaikiwa kurudi katika uhusiano na Mungu. Ingawa Mungu ndiye anayeachwa na mwanadamu kwa kumgeuzia kisogo, Yeye mwenyewe anakuwa ndiyo mwanzo mpya wa kuurejeza uhusiano mwema; anakuwa chanzo cha utakaso wake. Hapa ndipo tunapouona ukuu wa upendo wa Mungu kwetu.

Ni sababu gani Kristo anakuwa kwetu kielelezo cha upendo wa Mungu? Hili linaelezewa na Injili ya sherehe hii. Kristo anajitambulisha kama mwenye upole na unyenyekevu moyoni. Sifa hizi mbili mahsusi za kimungu ndizo zinautamalakisha upendo wa Mungu kwa wanadamu. Upole unamsukuma mtu kuingia katika uwanja wa mtu mwingine na kuonja hisia zake na kutembea naye; upole unamsukuma mmoja kuonja mateso ya mtu mwingine; na upole unamfanya mmoja kuwa mnyenyekevu. Kwa upande mwingine, unyenyekevu unatupatia fursa ya kuwasikiliza wengine; unawapatia fursa wengine kuonekana; unatuondolea kiburi na majigambo yetu na kuepa kuwadharau wengine; unyenyekevu unatuelekeza kuwa wapole na wenye subira.

Hizo ndizo tabia za kimungu ambaye anaangalia kujenga na si kubomoa; ambaye anaangalia kuuhisha na si kuua; anayeangalia kuganga na siyo kuharibu. Upendo huu wa kimungu kama tunavyoelezewa na Injili Takatifu unatuhitaji kujiweka mbele ya Mungu mithili ya mtoto mchanga mikononi mwa mzazi wake; unatudai kujitegemeza kwake na kuichota hekima yake. Ndiyo maana Kristo anatualika kwenda kujifunza huo upendo wake na kuufanya kuwa kawaida yetu. Huu ni mwaliko wa kuepukana na aina ya upendo ambao wana wa ulimwengu huu wanaukumbatia. Upendo wao wa nipe nikupe, upendo ambao unatafuta faida, upendo ambao unatafuta kupata. Moyo Mtakatifu Yesu ni kielelezo chetu cha namna tunavyopaswa kuhusiana na wenzetu katika hali zote. Kwa wale wanaokosa kuwaelekeza kwa upole na kwa wale wanaonenda vyema kuwaimarisha zaidi.

Mtume Yohane anatualika kujifunza Upendo huo kama uthibitisho wa upendo wetu kwa Mungu. Dini yetu inapata mantiki pale tunapoonesha upendo wa dhati kati yetu sisi kwa sisi. Kwani “ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana”. Upendo wetu kwa wenzetu ni udhihirisho wa uwepo wa Mungu ndani mwetu kwani “tukipendana Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu”. Matendo yetu mema kwa wenzetu ni matokeo chanya ya uwepo wa Mungu ndani mwetu. Mahali pengine Mtume Yohane anakuambia kwamba: “Mtu akisema ‘Nampenda Mungu’ naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo. Kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona” (1Yoh 4:20). Upendo wetu kwa Mungu unajifunua katika upendo wetu kwa jirani zetu.

Tunapouabudu Moyo wa Mtakatifu wa Yesu tunamaanisha tunamruhusu Mungu kuigeuza mioyo yetu kwa upendo wake mkuu na kuifananisha na Moyo huo Mtakatifu wa mwanae. Hapa tunataka upendo huo umiminike toka ndani mwetu na kuwaendea wengine katika mahusiano yetu sisi kwa sisi. Bila upendo huu wa kimungu hatuwezi kuishi sawasawa kama wana wa Mungu. Hivyo tuuchote upendo wa Mungu kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu; tuchote nguvu ya kujitoa na kuwagawia wengine vipawa vya Mungu tulivyokirimiwa hasa pale tunapopatwa na kigugumizi au uzito wa kushirikiana na wengine. Hii ni nyenzo muhimu kwetu na kushirikiana na ndugu zetu wote katika upendo wa Mungu kwani ibada yetu katika Moyo Mtakatifu wa Yesu inatuunganisha na Mungu. Yeye anakuwa ndani yetu nasi ndani yake.

Tuuabudu Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kuifanya mioyo yetu kufanana na Moyo wake. Tuiombe neema ya Mungu kusudi tuitambue thamini ya Moyo Mtakatifu wa Yesu na kuchota katika chemchemi ya neema anayotumiminia. Tuuadhimishe upendo wa Mungu na kuusimika katika jamii ya wanadamu kwa ajili ya wokovu wa watu wote.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.