2017-06-22 17:07:00

Papa Francisko asema, bado anajipanga, lakini Sudan iko moyoni mwake!


Mnamo tarehe 27 Oktoba 2016 Baba Mtakatifu Francisko alikutana na viongozi watatu wa Baraza la Makanisa la Sudani ya Kusini, mjini Vatican. Tangu hapo Baba Mtakatifu kaonesha ukaribu wa pekee katika kufuatilia hali za wananchi Sudani ya kusini. Mnamo tarehe 12 Aprili 2017, akaamua kushiriki katika kuwezesha miradi mitatu nchini humo kwa upande wa afya, ajira na elimu. Juhudi zinazojulikana kama “Baba Mtakatifu kwa ajili ya Sudani ya kusini”.

Kwa upande wa afya, kupitia Shirika la Masista wa Comboni, katoa msaada kwa ajili ya wafanyakazi na dawa kwa hospitali mbili. Hospitali ya kwanza ni ya Wau ndani ya jimbo la Wau, inayohudumia takribani wagonjwa 40,000 kwa mwaka, na wastani wa wajazito 6 wanaojifungua kwa siku. Pili ni Hospitali ya Nzara iliyopo kwenye jimbo la Tombora-Yambio inayohudumia wastani wa wagonjwa 90 kwa siku. Kwa upande wa ajira kumekuwa na misaada ya Sementi na pembejeo za kilimo kwenye majimbo ya Tombora-Yambio, Yei, Torit, Malakai na Juba ambapo familia 2,500 zilipokea misaada hiyo kupitia Caritas. Kwa upande wa elimu, kumekuwa na miasaada kwa ajili ya kuandaa walimu, manesi, wataalamu wa kilimo na viongozi jamii, ambapo kumekuwa na wanafunzi 3,482 katika jimbo la Yambio.

Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu ya Binadamu, akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano, tarehe 21 Juni 2017, anasema, imekuwa hamu ya Baba Mtakatifu Francisko kwa muda sasa kutaka kwenda Sudani ya kusini. Hata baada ya kuwa amepanga hija yake ya kitume kwa mwezi Oktoba 2017, hivi karibuni imelazimika kuahirisha safari yake kutokana na hali kutokuwa nzuri kwa ugeni kama huo nchini humo. Pamoja na kushindwa kutimiza hamu ya moyo wake kwa siku za hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko, bado kapenda kuonesha ukaribu wake kwa kutoa misaada kwenye sekta za fya, elimu na ajira kupitia mashirika na tasisi mbali mbali za kikanisa na kimataifa.

Sudani ya kusini imeingia kwenye machafuko tangu 2013 na kujikuta nchi hiyo ikiangukia kwenye sintofahamu kubwa kuhusu mahitaji msingi ya binadamu. Vita ya wenyewe kwa wenyewe inaendelea kutafuna wahanga wengi nchini humo. Baa la ugonjwa wa kipindupindu, ukosefu wa chakula na zaidi ya watu milioni 7.3 wanafariki dunia, ubakaji kwa akina mama na watoto. Vifo na kukata tamaa kunawala wengi, kiasi kwamba mpaka sasa raia milioni moja na nusu wamelazimika kuikimbia nchi yao na kutafuta hifadhi nchi za majirani.

Baba Mtakatifu ni kiongozi kilimwengu ambaye hafungwi na mipaka. Anaguswa sana na uhitaji wa kuongoza mfano kwa Jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kushiriki kila mmoja kadiri ya nafasi na uwezo ili kutatua hali hiyo tete nchini Sudani ya kusini, ambapo inaonekana wengi kulifumbia macho na kulizibia kinywa, anasema Kardinali Turkson. Juhudi za “Baba Mtakatifu kwa ajili ya Sudan kusini” zinanuia kunyanyua maendeleo ya watu na kurudisha amani nchini humo.

Baba Mtakatifu hawasahau wahanga wa majanga mengi nchini Sudani ya kusini wanaoonekana kutosikilizwa na wanaendelea kuumia kimya kimya, kutokana na kinzani, nyanyaso za kinyama na umwagaji damu. Kupitia Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu ya Binadamu, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kutafuta namna ya kupatikana utulivu na amani nchini humo. Anaendelea kuwa karibu na watu wa Sudani ya kusini katika sala zake za kila siku, na zaidi sana bado ana matumaini makubwa ya kufanya hija ya kitume nchini humo mapema iwezekanavyo. Kanisa kwa matumaini makubwa, lina imani kwamba Mungu anao uwezo wa kutenda kile ambacho kwenye macho ya wengi kinaonekana kama hakiwezekani.

Na Padre Celestine Nynada.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.