Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Katekesi siku ya Jumatano

Watakatifu, Mashuhuda na wandani wa matumaini

Watakatifu, mshuhuda na wandani wa kuishi utakatifu. - ANSA

21/06/2017 13:12

Siku ya kupata Sakramenti ya Ubatizo kwa kawaida husomwa Litania ya watakatifu, ikiwa ni sala ya kuwaomba waweze kuwa wandani wa wakristo wapya katika kuishi kwa uaminifu imani yao. Watakatifu ni wandani wa waamini, kwani wao pia wamefanya hija ya maisha hapa duniani, wakajua mahangaiko na taabu zilizopo, lakini wakaweza kuvumilia na kushinda, na sasa wamo mikononi mwa Mungu wakiwaombea wale ambao bado wapo katika hija hiyo duniani. Kwa nmana hii Baba Mtakatifu kafungua Katekesi yake siku ya Jumatano, tarehe 21 Juni 2017, akiwaalika waamini kuwa jasiri na matumaini makubwa katika kuuchuchumilia utakatifu.

Waamini katika mapambano dhidi ya ubaya hawakati tamaa. Wakristo wanaamini kwamba ubaya na hila zote za yule mwovu haziwezi kushinda. Chuki, kifo, au vita sio neno la mwisho, kwani katika kila hatua ya maisha ya mwanadamu, mkono wa Mungu upo pamoja naye. Watakatifu pia, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kwa namna mmoja au nyingine wanashiriki katika mahangaiko ya wale ambao bado wapo kwenye hija ya maisha hapa duniani.

Katika Sakramenti ya ndoa pia, Litania ya watakatifu husomwa kuomba maombezi yao kwa ajili ya wale wanaofunga ndoa, ili waweze kuwa waaminifu katika upendo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuliko kuwa mdanganyifu ni heri kutokufunga ndoa na kuishi useja. Kwa wana ndoa wanapojikuta katika hali ngumu, wawakumbuke wale waliotangulia na wakafanikiwa kuwa waaminifu hadi mwisho, wakiosha mavazi yao kwa damu ya mwana kondoo (Rej. Ufunuo 7:14). Waamini waombe msaada wa watakatifu kwani watakatifu wamo katika hija ya maisha yao kila siku.

Makasisi pia wanakumbuka siku ya upadrisho wao, litania ya watakatifu husomwa wakiwa wamelala kifudifudi ambapo jeshi la Paradiso linakuwa mabegani mwao, kwani neema ya Mungu haipungui katika maisha na utume wao. Waamini ni mavumbi, na katika unyonge wao wanayainua macho juu kuelekea mbinguni kwa matumaini ya kuwa pamoja na watakatifu. Inawezekana kuwa mtakatifu katika maisha ya kila siku, hata hivyo ni muhimu kusali kila siku pia, anasema Baba Mtakatifu Francisko. Ni mwaliko kuomba neema ya Mungu ili kuishi kwa imani thabiti na matumaini ya kuwa watakatifu. Baba Mtakatifu kawaalika waamini kujiandaa kwa siku ya ijumaa, sikuku ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, siku iliyotengwa maalumu kwa ajili ya kuombea utakatifu wa mapadri. Kawaalika vijana kwa namna ya pekee kuchovya maisha yao katika kisima cha upendo wa Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, radio Vatican.

21/06/2017 13:12