2017-06-21 12:24:00

Papa Francisko kufanya hija ya kichungaji Chile na Perù, Jan. 2018


Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na viongozi wa Serikali na  Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Chile na Perù kumwomba ili aweze kutembelea katika nchi hizi, ili kuwaimarisha ndugu zake katika Kristo! Ratiba elekezi ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Chile inaonesha kwamba, atakuwemo nchini humo kuanzia tarehe 15 - 18 Januari 2018. Atabahatika kutembelea miji ya Santiago, Temuco na Iquique.

Baraza ka Maaskofu Katoliki Chile limepokea taarifa hii kwa moyo wa shukrani na furaha kubwa anasema Askofu mkuu Ivo Scapolo, Balozi wa Vatican nchini Chile. Huu ni muda muafaka kwa familia ya Mungu nchini Chile kukuza na kuimarisha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa upande wake, Askofu Santiago Jaime Silva Retamales, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Chile anasema, kwa sasa changamoto kubwa mbele yao ni kujenga na kudumisha Jamii inayofumbatwa katika upendo na mshikamano wa dhati; kwa kumwilisha tunu msingi za maisha na utume wa Kanisa.

Hii ni fursa makini ya kuendelea kutekeleza changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, yaani, waamini wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa familia ya Mungu nchini Chile. Kanisa nchini Chile, litapaswa kuandamana na Baba Mtakatifu Francisko, kwa kusikiliza na kumwilisha changamoto anazoendelea kulipatia Kanisa yaani: umoja na mshikamano; huruma na upendo unaomwilishwa miongoni mwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baraza la Maaskofu Katoliki Chile linapenda kujikita zaidi na zaidi katika ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika haki na amani. Kardinali Ricardo Ezzati anasema, ni furaha isiyokuwa na kifani kwa Baba Mtakatifu kutembelea Chile, mahali ambapo familia ya Mungu inaendelea kujizatiti katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Taarifa iliyotolewa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican inakazia kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 18 - 21 Januari, 2018 atakuwa nchini Perù. Huko anatarajiwa kutembelea miji ya Lima, Puerto Maldonado pamoja na Trujillo. Undani wa ratiba yenyewe utatolewa baadaye kwa  wakati muafaka! Kardinali Juan Luis Ciprian Thorne anasema, familia ya Mungu nchini Perù imepokea kwa furaha na moyo wa shukrani, taarifa ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao. Papa Francisko atakwenda nchini Perù kama hujaji wa haki, amani na umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.