2017-06-21 12:40:00

Mshikamano na ukarimu kwa makanisa hitaji kunalipendezesha Kanisa


Kutoa ni moyo sio utajiri. Kunapokuwa na haja ya kuwa na mshikamano na kufanya ukarimu kwa makanisa yanayohitaji, kinachotazamwa katika kutoa sio wingi wa vitu bali moyo mkunjufu na mkarimu katika kujitoa kuwahudumia wengine. Kwa namna hii, Kanisa la Korintho kwa enzi za mtume Paulo, ingawa lilikuwa Kanisa tajiri, lilijikuta likilegea kwenye kutoa mchango kwa ajili ya Kanisa mama la Yerusalemu, wakati Kanisa la Macedonia ambalo halikuwa na uwezo sana, lilijitoa zaidi. Hii ni sehemu ya mahubiri ya Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, siku ya Jumanne, wakati wa Misa Takatifu ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa 90 wa Shirika la Misaada kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, ROACO.

Huu ni mwaliko kujitafakari kila mmoja binafsi na katika vikundi na taasisi kuona mwenendo wa maisha, maamuzi, miradi na matendo iwapo yanaakisi matakwa ya Mwenyezi Mungu, na iwapo kila mmoja atakuwa na ujasiri wa kumtazama Kristo ambaye alijimimina kutoka katika utukufu na kujifanya maskini kati ya wanadamu ili mwanadamu apate wokovu na utajiri wa Ufalme wa Mungu (Rej. IIWakorintho 8: 9).

Ukarimu na mshikamano kati ya makanisa sio tu tendo la haki jamii, linaloleta usawa kati ya makanisa, usawa kati ya watu. Ukarimu na mshikamano huu kati ya makanisa hauna lengo la kumfanya fulani kuwa maskini au kumtajirisha mwingine, bali ni kufuata nyayo za Kristo na kubaki kuwa wafuasi waaminifu. Ni tendo la kuumega mkate katika Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, kugawana chochote kilichopo ili kila mmoja aweze kushiriki maisha yenye hadhi na heshima kwa utu wa mwanadamu.

Kardinali Sandri anasema, katika kutafakari kwa kina zaidi, mchango kwa ajili ya Kanisa mama la Yerusalemu kipindi cha mtume Paulo, ulikuwa ni mchango unaotoka kwa watu wa mataifa, walioongoka kutoka upagani wakawa wakristo, hali Kanisa la Yerusalemu lilikuwa ni Kanisa la wakristo wayahudi. Ufahamu huu usaidie kutambua umuhimu wa umoja na mshikamano, kwani kila mmoja kakutana na Kristo katika tamaduni tofauti, kati ya jamii zenye mtazamo tofauti, lakini waamini wote wanatengeneza Kanisa moja tu la Kristo.

Misaada kwa ajili ya makanisa ya mashariki, ni mwendelezo wa mwaliko wa mtume Paulo kushikamana na makanisa hitaji katika ukarimu. Kudumu katika umoja na mshikamano wa namna hii, kunazidi kulipendezesha Kanisa, ambalo ni mchumba wa Kristo. Katika mshikamano huu, Kardinali Sandri anawaalika waamini kukumbuka na kuishi agizo la Kristo: “wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni” (Rej. Luka 6:27).

Waamini nchini Siria, Iraq, Misri, na kwenye nchi ambako wengi wanakimbia na kuhamia nchi zingine sababu ya nyanyaso mbali mbali, wanaalikwa kuishi fundisho hili kwa kina, pamoja na ukweli kwamba lina ugumu wake. Lakini ndivyo yalivyo maisha ya mfuasi wa Kristo, ni maisha ya msalaba, ambao sio wa kutupa, bali wa kuubeba mpaka mwisho. Kardinali Sandri, kawaweka waamini wote wanaoteseka na wale wanaojitoa ili kuwahudumia makanisa yanayoteseka, katika tunza na maombezi ya Mama Bikira Maria, na Wafiadini wa hivi karibuni waliomwaga damu katika nchi kama hizo.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.