2017-06-20 17:05:00

Papa Francisko: Injili ya Kristo iwe ni chachu ya kulinda utu wa watu


Akitoa Hotuba yake wakati wa Hija ya Kitume huko Barbiana, Italia, Jumanne, tarehe 20 Juni 2017 Baba Mtakatifu Francisko amesema kwamba, kafanya hija hiyo kwa heshima ya kumbukumbu ya Padre Lorenzo Milani, padre aliyetolea ushuhuda ni jinsi gani kupitia kujitoa kwake kwa Kristo, ndugu wanakutana na kuhudumiana katika mahitaji yao, ili kutetea, kulinda na kukuza heshima kwa utu wa binadamu. Baba Mtakatifu Francisko kaonesha furaha kwa kukutana na baadhi ya waliokuwa wanafunzi wa Padre Lorenzo Milani, alipokuwa Parokiani San Donato Calenzano kama mwalimu wa imani kwa waamini wote, lakini pia alipopelekwa shule ya Barbiana kufundisha somo la Fasihi Andishi.

Padre Lorenzo Milani alipohamishiwa shuleni hapo, hakutenganisha upadre na ualimu, bali alitambua kuwa ni huduma moja anayopewa na Kristo, ambapo amekabidhiwa watoto ili awalee na kuwakuza kwa upendo, na ndivyo alivyofanya. Kwa jamii kama ya nyakati za padre huyo, ni jamii ya sasa, ambapo katika utendaji wote, kuna haja kubwa ya kushikiria na kuishi Neno la Mungu kama upanga wenye makali kuwili, ili kupambanua ukweli kati ya nadharia nyingi zinazopepea hewani siku hizi, anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kwa namna hii waamini wataweza kurudisha haki kati ya watu, na kufanya kila mmoja kuishi kidugu.

Akitoa shukrani kwa walimu na walezi wa vijana waliokuwepo wakati wa Hotuba yake huko Barbiana, Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba huo ni wito, sio tu wa kufundisha, bali pia wa kuwapenda vijana wanaowafundisha na kuwalea. Kwa namna ya pekee, ni mwaliko wa kila mmoja kuzingatia malezi bora kwa vijana wa kizazi kipya, hasa wanaoishi katika mazingira hatarishi kiuchumi, kiutandawazi, na kinzani mbali mbali.

Baba Mtakatifu Francisko kawaalika mapadri kuzidi kujitoa na kujimimina kwa ajili ya huduma kwa watu, wakikumbuka kwamba zawadi ya upadre kwanza kabisa inatanguliwa na zawadi ya imani na upendo kutoka kwa Kristo mwenyewe. Kwa kuonjeshwa upendo wa Kristo, mapadri wanaalikwa kuvutwa zaidi katika kumtafuta Mungu kama alivyofanya Padre Lorenzo Milani, kwani bila hamu ya kumtafuta Mungu, wataishia kuwa watendaji maafisa kanisani lakini sio watumishi wa Mungu mapadri. Kwa kasisi yeyote, uchaji wa Mungu, maisha ya sala, upendo, ukarimu na huruma ya kibaba katika utume ndivyo vinavyompambanua.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, uwepo wake Barbiana siku ya jumanne, na kitendo cha kusali mbele ya kaburi la Padre Lorenzo Milani, ni ishara ya nguvu ya kutambua utakatifu wa maisha yake, na utume alioufanya kwa Kanisa hasa kwa kupigania maskini na wanyonge. Hata hivyo Baba Mtakatifu Francisko kasema, hiyo haifuti ukweli kwamba, padre huyu alipata mahangaiko mengi na kuteseka kutoka kwa viongozi wa Kanisa sababu hakueleweka vizuri kipindi hicho. Jambo la msingi zaidi, ni kujifunza kutoka kwenye uthabiti wa imani yake na utii, uliomsukuma kuendelea kujitoa kwa huduma kati ya watu bila ya kujibakiza.

Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.