2017-06-20 06:58:00

Kard. Basseti: Hakuna mtu wa kuja, wote wanaunda familia ya binadamu!


Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi Barani Ulaya na Amerika katika ujumla wake, linaendelea kukumbana na kisiki cha mpingo, kwa baadhi ya nchi kuweka sera za kujenga kuta za ubaguzi zinazowatenganisha watu! Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, baadhi ya wanasiasa wanaotaka kujijengea umaarufu kitaifa na kimataifa wamekuwa wakieneza hofu na mashaka kwa wananchi wao juu ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kuwa ni watu hatari sana wanaoweza kusababisha mashambulizi ya kigaidi hivyo kuhatarisha ulinzi na usalama!

Wanasiasa hao wanasema, hawa ni watu hatari wanaotaka kuwapoka fursa za ajira na hivyo kuongeza kasi ya umaskini na ukosefu wa fursa za ajira. Kardinali Gualtiero Basseti, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia anasema, watu wanakosa utu na heshima kwa wakimbizi na wahamiaji wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali! Hawa ni watu wanaopaswa kuthaminiwa utu na  heshima yao, kupewa hifadhi na kushirikishwa katika mchakato wa maisha ya Jamii husika.

Ni wajibu wa wanasiasa na Kanisa katika ujumla wake, kuwaelimisha waamini pamoja na wananchi kuhusu utajiri mkubwa unaobebwa na wahamiaji pamoja na wakimbizi na kwamba, hawa si kero wala tishio la maisha; dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa umakini mkubwa kwa kujikita katika tunu msingi za Kiinjili kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko mintarafu wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji ni sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayojika katika utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi yanayoweza kutekelezwa kwa njia ya mshikamano wa dhati unaoongozwa na kanuni auni!

Huu ni urithi mkubwa wa Kanisa Katoliki kutoka kwa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, dira na mwelekeo wa kichungaji kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika kipindi cha miaka kumi kuanzia sasa. Mwenyeheri Paulo VI katika hotuba yake ya kuhitimisha maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican alikazia utu na heshima ya binadamu tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Lengo anakaza kusema Mtakatifu Yohane Paulo II ni kutangaza na kushuhudia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na Papa Francisko anasema, hawa ni watu wanaopaswa kuoneshwa huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kikomo!

Kardinali Gualtiero Basseti anakaza kusema, Kanisa Katoliki limekuwa na utamaduni na mapokeo hai ya kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, licha ya kwamba, dhana ya uhamiaji inapata chimbuko lake kutoka katika Agano la Kale na Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ilionja adha ya kukimbilia uhamishoni ili kusalimisha maisha ya Mtoto Yesu aliyekuwa anatafutwa na Mfalme Herode! Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Maaskofu kama vile: Giovanni Maria Scalabrini na Geremia Bonomelli na hatimaye, Papa Pio X akaanzisha Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kunako mwaka 1914 wakati wa vuguvu la Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Mwenyeheri Paulo VI tarehe 19 Machi 1970 akaanzisha Tume ya Wakimbizi na Wahamiaji ambayo kunako mwaka 1988, Mtakatifu Yohane Paulo II akaibadilisha na kuwa ni Baraza la Kipapa la wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, Baraza ambalo kwa sasa ni sehemu ya Baraza la Kipapa la Huduma Endelevu ya Maendeleo ya Binadamu, sehemu ya mageuzi makubwa yanayoendelea kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko. Hili ni Baraza linaloendelea kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili; urithi mkubwa wa kutoka kwenye Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kuendelezwa na wakuu wa Kanisa waliofuatia tangu wakati huo!

Kardinali Gualtiero Basseti anasisitiza kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tangu mwanzo wa utume wake, ameonesha kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wakimbizi na wahamiaji katika maisha na utume wake, kwa kuguswa na utu wa watu hawa waliokuwa wanakufa maji baharini, kashfa kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa ambayo hadi leo imeendelea kuwa ni chanzo cha kuwagawa na kuwasambaratisha, wakati bado watu wanaendelea kupoteza maisha katika kilindi cha bahari ya Mediterrania. Hili ni kaburi lisiokuwa na alama yoyote.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kisiwa cha Lampedusa, Kusini mwa Italia, ilitafsiriwa na wengi kuwa ni tukio la kihistoria ambalo limeacha alama ya kudumu katika akili na nyoyo za watu! Mwenyeheri Paulo VI anasema, ndani ya Kanisa hakuna “mgeni”, “mtu wa kuja”, “mnyamahanga” au “kiyasaka” bali wote wanaunda Jumuiya moja ya binadamu inayopaswa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana wakati wa raha na machungu! Vinginenvyo anasema Kardinali Gualtiero Basseti, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia, Italia, dunia itaendelea kugawanyika katika kundi A wanaopaswa kupewa kipaumbele cha pekee na dunia kundi B, linaloweza kuachwa kupotea na kusambaratika katika uso wa dunia kutokana na umaskini, magonjwa, njaa, maradhi na vita! Kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba, wao ni bora zaidi kuliko wengine; badala ya kuwa ni watu wenye utu na heshima yao, wanageuzwa kuwa ni vyombo na vichokoo vya kuridhisha tamaa za binadamu pamoja na kuendeleza utumwa mamboleo, kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu, mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha kwanza katika Mafundisho Jamii ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.