2017-06-19 11:15:00

Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu!


Waamini wa Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, Jumapili tarehe 18 Juni 2017 wameadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu kama inavyojulikana na wengi: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini. Kila Jumapili, waamini wanaadhimisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, iliyoanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe, Siku ile ya Alhamisi kuu wakati wa Karamu ya Mwisho! Lakini, kila mwaka, Kanisa lina furaha kubwa ya kuadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu, kiini cha imani ya Kanisa kwa kumwabudu Kristo Yesu anayejisadaka na kujitoa kwa waja wake kama chakula na kinywaji cha wokovu!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 18 Juni 2017, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kristo Yesu ni mkate na kinywaji kilichoshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele; ni sadaka ya Kristo mwenyewe kwa ajili ya binadamu! Mwana wa mtu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu ni Mwana Kondoo wa Pasaka, anayemkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa lindi la dhambi na mauti na kumwongoza katika Nchi ya ahadi.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili  kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki na amani.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, huu ni uwepo endelevu wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu unaofumbatwa katika maisha ya waamini mahali popote pale walipo: mjini na vijijini; Kaskazini na Kusini mwa dunia; katika nchi ambazo kimsingi zina utamaduni na Mapokeo ya Kikristo na hata katika Nchi zile ambazo zimeinjilishwa hivi karibuni. Katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, Yesu anajisadaka mwenyewe kama nguvu ya maisha ya kiroho ili kuwajengea uwezo wafuasi wake wa kumwilisha Amri ya upendo: kwa kupenda kama alivyopenda Yeye mwenyewe; kwa kujenga na kudumisha jumuiya inayomsimikwa katika ukarimu, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, kulishwa na Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni kujiaminisha kwake na kumwachia nafasi ili aweze kuwaongoza. Huu ni mwaliko wa kumpokea na kumpatia Kristo Yesu nafasi ya kwanza katika maisha, tayari kupokea na kumwilisha upendo unaobubujika kutoka katika umoja wa Fumbo la Ekaristi Takatifu, dhamana ya Roho Mtakatifu anayerutubisha na kuimarisha upendo kwa Mungu na jirani; watu wanaokutana nao kila siku ya maisha yao! Kwa kulishwa na kunyweshwa Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu, waamini wanakuwa kweli ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kwa kuhamasishwa kujenga na kudumisha umoja na upendo vinavyobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu kama ambavyo waamini wanavyokumbushwa na Mtakatifu Paulo, Mtume! Ekaristi Takatifu ni kifungo cha upendo na umoja. 

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumwomba Bikira Maria, aliyejifungamanisha daima na Kristo Yesu Mkate wa uzima, akawa Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ili aweze kuwasaidia kutambua, kugundua na kurutubishwa kwa njia ya imani na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, ili hatimaye, waweze kujenga na kudumisha umoja na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao katika Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.