2017-06-19 14:27:00

Mwezi wa kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa


Mama Kanisa anaendelea kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, yatakayotimua vumbi mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani kwa njia ya maisha na wito wa kitawa na kipadre pamoja na kufanya maamuzi magumu ya maisha na wito wa ndoa, yote yawe ni kwa ajili ya kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yao!

Itakumbukwa kwamba, Mwezi Juni, Kanisa limeutenga kwa namna ya pekee kwa ajili ya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ni Moyo uliotobolewa na humo zikatoka Sakramenti za Kanisa, yaani: Sakramenti ya Ubatizo na Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mapadre na watawa wamekumbushwa kwa namna ya pekee kuwa, wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, unaobubujika kutoka katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na kwa namna ya pekee, Fumbo la Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho.

Watawa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa njia ya sadaka na huduma makini wanayoitoa kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia katika elimu, afya, ustawi na maendeleo ya jamii! Familia nazo zinakumbushwa kwamba, ni Kanisa dogo la nyumbani, chemchemi na kitalu cha miito mitakatifu; ni shule ya sala, maadili na utu wema! Ni mahali pa kusaidiana, kurekebishana na kushikamana katika kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya tunu msingi za maisha ya Kikristo na utu wema! Kwa njia hii, Kanisa linaendelea kuwa kweli ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Matiafa!

Baraza la Maaskofu Katoliki Uruguay, kwa kutambua na kuthamini mchango wa mapadre na watawa katika maisha na utume wa Kanisa, hasa katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, limeamua kutenga Mwezi Juni 2017 kuwa ni mwezi wa kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa, yaani: wito wa upadre, ili Kanisa liweze kuwapata Mapadre: wema na watakatifu; wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kugawa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Kanisa nchini Uruguay linawaombea wanafamilia ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao kikamilifu katika maisha na utume wa ndoa na familia, kwa kutambua kwamba, ndoa na familia zinakabiliwa na changamoto pevu, pasi na sala, udumifu, huruma na upendo wa Mungu zinaweza kujikuta zinaogelea kwenye dimbwi la tope!

Mwezi wa Kuombea Miito nchini Uruguay, unaongozwa na kauli mbiu “Mimi ni Yule ambaye anazungumza nawe”. Majimbo yote nchini Uruguay hayana budi kuwasaidia waamini kutambua wito na dhamana yao katika maisha na utume wa Kanisa kadiri ya mpango wa Mungu kwa kila mmoja wao. Padre Mauro Fernàndez, Katibu mtendaji wa Idara ya Miito Jimbo kuu la Monteverde nchini Uruguay anasema, wito ni dhana pana zaidi katika maisha na utume wa Kanisa. Licha ya kuombea miito mitakatifu, lakini ikumbukwe kwamba, wito wa kwanza unafumbatwa katika Injili ya uhai; maisha ya Kikristo na Utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, chachu makini ya uinjilishaji mpya!

Waamini wanaalikwa kutambua na kuonja upendo wa Mungu katika safari ya maisha yao ya kila siku, ili kuweza kujibu kwa ukarimu. Maadhimisho ya Mwezi wa Miito nchini Uruguay, yalizunduliwa hivi karibuni na Kardinali Daniel Sturla, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Monteverde. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuhakikisha kwamba, wanatekeleza Amri ya Kristo ili kusali na kumwomba Bwana wa mavuno aweze kupeleka watenda kazi katika shamba lake! Kanisa linahitaji watenda kazi wema, watakatifu, wachapakazi, waadilifu na wachamungu; watu ambao wako tayari kuambatana na familia ya Mungu kwa wakati wa raha na machungu!

Mwezi Juni, 2017, Kanisa linaendelea kuwahamasisha vijana wa kizazi kipya kufanya maamuzi machungu katika maisha yao: kwa kutambua wito wao ili waweze kujibu kwa ukarimu na ujasiri kama alivyofanya Bikira Maria, leo hii vizazi vyote wanamwita Mwenyeheri, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amemtendea makuu na huruma yake hudumu kizazi baada ya kizazi! Kanisa kwa njia ya ushuhuda na maelezo ya Mapadre na walezi na wataalam mbali mbali wanaendelea kuwasaida vijana kutambua wito wao na kwamba, Kanisa lina matumaini makubwa kwa sala inayotolewa kwa ajili ya kuombea miito mbali mbali ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.