Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu endelevu ya imani na mapendo!

Ekaristi takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya imani, matumaini na mapendo ya Mungu kati ya watu wake!

19/06/2017 10:59

Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu ya Pasaka ya Kristo, ni utekelezaji wa matoleo minthili ya Sakramenti ya Sadaka yake moja, katika Liturujia ya Kanisa ambalo ni Fumbo la Mwili wake. Ni kumbu kumbu  endelevu inayotangaza maajabu yaliyotendwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya watu wake “fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi”. Ni ukumbusho wa Pasaka, mwenyezi Mungu alipowakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri. Katika Agano Jipya, kumbu kumbu hii hupata maana mpya. Mama Kanisa anapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu anafanya ukumbusho wa Pasaka ya Kristo, aliyejisadaka mara moja tu Msalabani na kila mara Fumbo hili linapoadhimishwa, kazi ya ukombozi inaendelea kutekelezwa.

Kwa ufupi, Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya upendo wa Mungu kwa binadamu, kwani Kristo Yesu ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni. Liturujia ya Neno la Mungu katika maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu yanawakumbusha waamini jinsi ambavyo kumbu kumbu hii imefanyika mwili katika mchakato mzima wa kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwani, wakaishi jangwani kwa muda wa miaka arobanini, chemchemi ya historia ya ukombozi wa mwanadamu. Ni wajibu kwa waamini kukumbuka mambo msingi katika imani, ili hatimaye, waweze kuzaa matunda katika maisha yao ya kiroho. Imani inafumbatwa katika kumbu kumbu hai ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, Sherehe ya Ekaristi Takatifu, Jumapili tarehe 18 Juni 2017, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane Wa Laterano, mjini Roma. Mara tu baada ya maadhimisho ya Misa takatifu, yalifutia maandamano ya Ekaristi Takatifu na hatimaye, baraka ya Ekaristi Takatifu iliyotolewa na Baba Mtakatifu mbele ya Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu. Ni maandamano yaliyosheheni sala na nyimbo za kumwabudu Kristo Yesu katika Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee, kumbu kumbu inayowawezesha waamini kubaki wakiwa wameshikamana katika upendo, kwa kuhifadhi kwenye sakafu ya moyo; kwa kumkumbuka yule anayewapenda upeo na kwamba, hata wao wanahimizwa kupenda. Jambo la kusikitisha anasema Baba Mtakatifu ni hali ya kupenda inaendelea kufifia  kutokana na watu kutaka kuzama katika mambo mapya, hali inayowafanya kushindwa kuzama kabisa katika undani wa imani yao, hali inayodhohofisha imani kutoka katika mizizi yake.

Sherehe ya Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu inayomwonesha Kristo Yesu anayekuja kuwatembelea waja wake katika hali ya upendo lakini katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.Yesu anawatembelea waja wake katika maumbo ya mkate wa uzima wa milele, ili kuwakumbusha waamini kumbu kumbu ya Mateso na Kifo chake Msalabani; upendo wa Mungu kwa waja wake, ambao kimsingi ni nguvu yao inayowategemeza katika safari ya maisha, ndiyo maana Mama Kanisa anahimiza kumbu kumbu endelevu ya Ekaristi Takatifu; kumbu hii ni hai na ni sehemu ya upendo wa Mungu unaofariji. Ekaristi Takatifu inafumbata maneno na matendo ya Kristo Yesu; inawaonjesha waamini Fumbo la Pasaka, yaani mateso yake na Roho wake. Waamini wanapompokea kwa imani na uchaji wanakuwa na uhakika kwamba, wanapendwa na Kristo.

Kwa namna ya pekee kabisa, upendo wa Kristo unajionesha miongoni mwa watoto waliopokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza katika maisha yao nao walikuwa ni wengi katika Ibada hii ya Misa Takatifu. Ekaristi Takatifu inawaundia waamini kumbu kumbu ya shukrani, kwani wanajitambua kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Baba wa milele! Hii ni kumbu kumbu huru kabisa, kwani upendo na msamaha wa Yesu unaganga na kuponya madonda na majeraha ya zamani na kuleta amani moyoni mwa waamini.

Hii ni kumbu kumbu yenye uvumilivu kwani hata katika magumu ya maisha, bado waamini wanatambua kwamba, Roho wa Kristo yuko ndani mwao. Ekaristi Takatifu inawatia shime kusonga mbele kwani hata katika safari ambayo ni ngumu kiasi gani, waamini wanatambua kwamba, hawako pweke, na kamwe Kristo Yesu hawezi kuwageuzia kisogo na kwamba, kila wakati wanapomwendea anawapatia nguvu mpya kwa njia ya upendo wake. Ekaristi Takatifu inawakumbusha waamini kwamba, hawapo peke peke, bali ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa; familia ya Mungu kama ilivyojionesha kwenye Agano la Kale ilipokusanyika kwa ajili kuokota manna iliyoshuka kutoka mbinguni.

Yesu ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni, anawaalika waamini kumpokea kwa pamoja na kumshikiri kati yao. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Umoja, inayowaunganisha waamini kuwa ni mwili mmoja na watu watakatifu wa Mungu. Mwamini anayepokea Ekaristi takatifu anakuwa ni chombo cha umoja, kwani ndani mwake kunaibuka “vinasaba ya maisha ya kiroho” vinavyosaidia kujenga umoja. Mkate wa Umoja unasaidia kuvunjilia mbali tabia ya kujiona kuwa ni bora zaidi kuliko wengine; watu wanaopenda kuwagawa wengine kwa mafao binafsi; watu wenye wivu na umbea unaohatarisha umoja na mshikamano. Waamini kwa njia ya kuishi kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu: wana mwabudu na kumshukuru Kristo Yesu, kwa zawadi hii kubwa; kumbu kumbu hai ya upendo wake unaowaunganisha wote kuwa ni mwili mmoja na kuwaelekeza katika ujenzi wa umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

19/06/2017 10:59