2017-06-17 17:35:00

Zaidi ya watu 100 wanahofiwa kufa kutokana na ajali ya moto London!


Watu zaidi ya 100 wanahofiwa kufariki dunia, wengine 24 wamelazwa hospitalini huku hali zao zikiwa mbaya na wengine 76 bado hawajulikani mahali walipo baada ya Ghorofa la Grenfell Tower” iliyoko Jijini London, kuungua moto na kuteketea kabisa, Jumatano, tarehe 14 Juni 2017. Tayari viongozi mbali mbali wa Uingereza wametembelea eneo la tukio na kuwafariji waathirika. Serikali ya Uingereza imeamua kutoa kiasi cha Paundi milioni tano kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa janga hili la moto.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican kwenda kwa Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales anasema, amesikitishwa sana na taarifa za janga la moto lililotokea hivi karibuni Jijini London na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Anapenda kuchukua nafasi hii kuwaombea wale wote waliopoteza maisha yao ili waweze kupata  pumziko la milele na majeruhi kupata nafuu na hatimaye kuweza kuendelea na shughuli zao. Baba Mtakatifu anawasifu na kuwapongeza wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya wahanga wa janga hili la moto ambao umeteketeza Jumba la ghorofa 24, likiwa na watu kadhaa ndani yake. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua nafasi hii kuiombea Uingereza nguvu na amani katika kipindi hiki kigumu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.