Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Sherehe ya Fumbo la Ekaristi Takatifu!

Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu na ushuhuda wa imani tendaji. - ANSA

17/06/2017 09:24

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Neno la Mungu, ambapo leo tunaadhimisha Sikukuu ya Mwili na Damu ya Kristo. Sakramenti hii iliwekwa na Kristo siku ya Alhamisi kuu, wakati wa karamu yake ya mwisho. Kwa kuwa wakati huo Kanisa huwa linakuwa kwenye kipindi cha kuadhimisha Fumbo la mateso ya Bwana, sikukuu hii huwa inaadhimishwa kwa kiasi, ili kuheshimu pia Fumbo la mateso ya Bwana. Hivyo Kanisa linapenda kuadhimisha katika Dominika hii, ili kutoa nafasi ya kutosha kusherehekea kwa shamra shamra zawadi hii ambayo Kristo kawaachia wafuasi wake. Karibu tutafakari kwa pamoja uzito wa zawadi hii na umuhimu wa shamra shamra za hadhara.

Mwili na Damu ya Kristo ni fumbo ambalo linapokeleka kwa jicho la Imani thabiti, kwani kinachoonekana kwa macho ya nje ni maumbo ya mkate na divai, hali kiini cha maumbo hayo kinakuwa kimegeuzwa na kuwa Mwili na Damu ya Bwana. Anayefanya muujiza huu, ni Krsito Mwenyewe (kupitia mikono ya makasisi wake), ambaye kwa njia yake vitu vyote vimeumbwa, wala pasipo Yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika (Rej. Yohane 1:3). Hivyo kwa uwezo alionao wakuumba vinavyoonekana na visivyoonekana, katenda Fumbo hili kubwa kuwa zawadi kwa maisha ya waamini.

Hii ni zawadi ya uzima, sababu kama tulivyosikia katika Injili, Yeye Mwenyewe anasema: Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho (Rej. Yohane 6:54). Mwili wa mwanadamu unahitaji chakula ili aweze kuishi na kuwa na afya bora, na Mwenyezi Mungu kamjalia viumbe ambavyo kutoka kwavyo anajipatia chakula cha mwili. Hata hivyo mwanadamu kaumbwa mwili na roho, hivyo uzima wa roho ya mwanadamu unahitaji chakula pia, ambacho ndio Mwili wa Kristo. Na uzima huo wa roho unadumu hata baada ya kifo cha mwili. Tunafahamu katika ufufuo wa Lazaro, Bwana anamwambia Martha: Mimi ndimi huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa, atakuwa anaishi (Rej. Yohane 11:25).

Mwanadamu baada ya kuumbwa kutoka mavumbini, alipuliziwa pumzi ya uhai na Mwenyezi Mungu, ndipo akawa mtu hai (Rej. Mwanzo 2:7). Hivyo kwa kuwa uzima wa roho ya mwanadamu ni uzima utakanao na pumzi ya Mwenyezi Mungu, kuishi kwa kiwango cha pumzi hiyo ya kimungu, kunahitaji mwanadamu abaki katika muungano na Mungu katika Utatu Mtakatifu.

Baada ya kuasi, mwanadamu akajitenga na muungano huo. Kristo anafanyika mwili, Mungu-mtu, anakuwa daraja la kuurudisha muungano huo kati ya Mungu na mwanadamu. Zawadi hii ya Ekaristi Takatifu humuunganisha mwanadamu katika umoja wa kina na Muumba wake, kama tulivyosikia katika Injili: Aulaye mwili wangu, na kuinywa damu yangu, hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, mimi ni hai kwa Baba, na kadhalika mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi (Rej. Yohane 6: 56-57).

Ndugu msikilizaji, katika kushiriki Ekaristi Takatifu kila mwamini anakuwa katika muungano na Mwenyezi Mungu, na kwa kuwa wote wanaoshiriki Ekaristi wanakuwa ndani ya Kristo, basi waamini wote wanakuwa katika muungano kati yao kupitia Kristo Mwenyewe aliye kiungo cha wote. Ndio sababu tumemsikia mtume Paulo akihoji kwa kukumbusha: Nasema kama na watu wenye akili, lifikirini ninyi ninenalo. Kikombe kile cha Baraka tukibarikicho, je! si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa Mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja (Rej. IWakorintho 10: 15 – 17). Kwa namna hii, taabu na mateso ya mwamini mmoja inakuwa ya wote, na furaha ya mmoja inakuwa furaha ya wote, sababu wameungana katika Upendo wa Ekaristi Takatifu.

Kanisa linapoadhimisha sikukuu hii ya Mwili na Damu ya Kristo, huzunguka katika njia mbali mbali, ikiwa ni sehemu ya kuonesha shukrani na kuthamini zawadi hii ambayo Kristo kapenda kumwachia mwanadamu na kubaki kaungana naye. Maandamano ya Ekaristi ni sehemu ya kuonesha kuwa tunamwabudu Kristo mbele ya ulimwengu wote, Yeye aliye Muumba wa vyote, kwa kuwa pale katika maumbo ya mkate, sio mkate tena bali ni Kristo Mwenyewe, Bwana wa mabwana, Mfalme wa wafalme, anayestahili heshima na utukufu wote.

Maandamano ni sehemu ya kumshuhudia Kristo kwa wale wasiomfahamu bado, au walimfahamu na baadae wakampotezea, iwe ni ishara ya mwamsho wa dhamiri zao wamrudie Muumba wao kwa utakatifu wa maisha. Maandamano haya kwa waamini yana maana yenye kina zaidi, kwani ni ishara ya kwamba wanaishi na Kristo katika shughuli na maisha yao ya kila siku, katika njia zile wanamopita na kuishi kila siku, kwani Kristo yumo ndani yao, hivyo ni hamasa ya kuishi kadiri ya mafundisho yake Kristo, kila wanapojikuta, wakifahamu kwamba yupo pamoja nao kila mahali.

Ndugu msikilizaji, nashukuru sana kuwa pamoja nami katika kipindi hiki, napenda kukukaribisha tena kwa kipindi kijacho cha tafakari ya Neno la Mungu. Nikuhimize tu kwamba, ujenge tabia ya kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na waamini wenzio, lakini pia wewe binafsi mahali ambapo kuna nafasi hiyo. Kumbuka tu kwamba, ni nafasi ya kuzungumza na Muumba wako kama rafiki wa kweli (Rej. Yohane 15:15), ambapo una uhuru wa kusema naye unavyojisikia, naye huzungumza nawe ndani ya dhamiri yako.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

17/06/2017 09:24