2017-06-17 16:13:00

Mtumishi wa Mungu Teresio Olivelli ni kati ya Wenyeheri watarajiwa


Mtumishi wa Mungu Teresio Olivelli, mwamini mlei aliyezaliwa kunako tarehe 7 Januari 1916, akasaidiwa katika malezi na makuzi yake ya kiroho; akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kukoleza utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wasomi; akawa kweli ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa maskini, wagonjwa na wazee! Akasimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Akakataa katu katu kushirikiana na utawala wa Kinazi na badala yake, akaonesha uaminifu na udumifu katika tunu msingi za Kiinjili na hatimaye, akauwawa kikatili kutokana na chuki za kidini tarehe 17 Januari 1945. Huu ni ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake!

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Ijumaa, tarehe 16 Juni 2017 ameridhia kwamba, Mtumishi wa Mungu Teresio Olivelli ambaye ameonesha ushujaa wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, kumbe, anaweza kuendelea na mchakato wa kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri, kadiri ya mpango wa Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia pia wafuatao kuendelea na mchakato wa kutangazwa kuwa Wenyeheri nao ni: Mtumishi wa Mungu Giuseppe De Sousa Barroso, Askofu wa Jimbo Katoliki Porto, aliyezaliwa kunako tarehe 5 Novemba 1845 na kufariki dunia tarehe 31 Agosti 1918. Kanisa lumetambua karama za kishujaa zilizooneshwa na Mtumishi wa Mungu Giuseppe di Gesù Lòpez y Gonzàlez, Askofu wa Jimbo Katoliki la Aguas Calientes na muasisi wa Shirika la Watawa Wakatoliki wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, aliyezaliwa kunako tarehe 16 Oktoba 1872 na kufariki dunia tarehe 11 Novemba 1950.

Baba Mtakatifu ametambua pia karama za kishujaa zilizoneshwa na Mtumishi wa Mungu Agostino Ernesto Castrillo, Askofu wa San Marco Argentano Bisignano, aliyzaliwa tarehe 8 Februari 1904 na kufariki dunia 16 Oktoba 1955. Mwingine ni Mtumishi wa Mungu Giacomo da Balduina, aliyefahamika pia kama Beniamino Filoni, Padre na Mtawa wa Shirika la Wakapuchini, aliyezaliwa tarehe 2 Agosti 1900 na kufariki dunia tarehe 21 Julai 1948. Kanisa limetambua karama za kishujaa zilizoneshwa na Mtumishi wa Mungu Maria degli Angeli, aliyezaliwa tarehe 16 Novemba 1871 na kufariki dunia tarehe 7 Oktoba 1949. Mwishoni, Kanisa limekiri karama za kishujaa zilizooneshwa na Mtumishi wa Mungu Umiltà Patlàn Sànchez, aliyejulikana pia kama Maria, Mtawa wa Shirika la Bikira Maria Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, aliyezaliwa kunako tarehe 17 Machi 1895 na kufariki dunia tarehe 17 Juni 1970.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.