2017-06-17 08:19:00

Mchakato wa kukabiliana na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji!


Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu limekamilisha semina maalum ya siku mbili kuanzia tarehe 12- 13 Juni 2017, iliyojadili kwa kina na mapana kuhusu changamoto ya wahamiaji, wakimbizi pamoja na waathirika wa biashara haramu ya binadamu. Semina hii imewashirikisha wajumbe 36 kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki 21; wawakilishi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican, wawakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa pamoja na Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, nchini Usswis.

Wajumbe wamepembua kwa kina na mapana changamoto ambazo zimejitokeza kwa sasa kutokana na kuibuka wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia; majibu ya dharura; sera na mikakati ya muda wa kati na muda mrefu; dhamana na mchango wa Kanisa katika ngazi mbali mbali; mchango wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume sanjari na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kikanda, Kimataifa na kitaifa. Wajumbe wamejikita zaidi katika maandalizi ya kile kinachoitwa “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji”.

Huu ni Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaolenga kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wahamiaji! Umuhimu wa Jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na maisha bora zaidi. Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa wahamiaji unapania pamoja na mambo mengine kuboresha: ulinzi na usalama; haki msingi za binadamu pamoja na kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria pale haki zao zinapovunjwa.

Mkataba huu unawatupia jicho wakimbizi na wahamiaji hatari kwa maisha na usalama wa raia wengine. Watu hatari wanaweza kurejeshwa makwao;  uwezekano wa kudhibiti uhuru wa wakimbizi. Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji” unapania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa kwa baadhi ya serikali pamoja na kuangalia umuhimu wa kutumia nguvu ya wakimbizi katika kuzalisha na kutoa huduma, mwishoni ni suala la udhibiti wa mipaka!

Haya ndiyo mambo msingi yaliyomo kwenye “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji”. Awamu ya kwanza ya majadiliano kuhusu Mkataba huu itafanyika huko Guadalajara, Mexico, mwezi Februari 2018. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Jukwaa la Wahamiaji na Amani, lililofanyika tarehe 21 Februari 2017 alikazia kwa namna ya pekee: ukarimu, ulinzi, ushirikishwaji na mwendelezo. Wajumbe wa semina hii wamejikita kwa namna ya pekee katika mambo msingi yanayopelekea makundi makubwa ya watu kuzikimbia nchi zao. Uhamiaji salama, unaojikita katika nidhamu; taratibu na uwajibikaji ni jambo linalowezekana ikiwa kama watu wataweza kuendelea kuishi katika nchi za asilia.

Kazi za Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ni kuyasaidia Mabaraza ya Maaskofu; Maaskofu mahalia, Mashirika ya Misaada ya Kimataifa, waamini na taasisi mbali mbali za Kanisa Katoliki zinazo jishughulisha na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; wanapokuwa njiani hadi pale wanapoingizwa rasmi katika nchi inayowapokea au wanapoamua kurejea tena makwao. Semina hii imekuwa ni nyenzo msingi ya kuiwezesha Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kutekeleza dhamana na wajibu wake. Wajumbe wamesikiliza shuhuda za wahanga wa wimbi la wakimbizi na wahamiaji.

Idara hii kwa sasa itaendelea kutoa huduma zake kwa njia ya mitandao ya kijamii ili kushirikishana kwa haraka zaidi: rasilimali watu, fedha na vitu wakati wa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Mkazo umewekwa katika ushirikiano kwa ajili ya kutekeleza malengo na huduma inayotolewa kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji. Matokeo ya semina hii yamekuwa ni makubwa kuliko hata matarajio yake. Changamoto za wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji zinaweza kushughulikiwa kwa umoja na ushirikiano; kwa kuvuka kinzani na migogoro; ili kuwajengea watu matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.