Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Maisha ya unabii ya mapadri Lorenzo Milani na Primo Mazzolari

Don Lorenzo Milani na Padre Primo Mazzolari walikuwa ni manabii katika maisha na utume wao!

17/06/2017 14:17

Padre Lorenzo Milani ni padre wa Kanisa katoliki aliyepadirishwa mnamo mwaka 1947 na kupangwa kuhudumia parokia ya Mtakatifu Donatus, huko Calenzano nchini Italia. Mwaka 1954 alilazimika kuamishiwa Barbiana maeneo ya Toscana, ikiwa ni namna ya kumthibiti kwa kumdhania kuwa anataka kuleta mageuzi ya maisha ya kipadri na imani katoliki. Ni padre aliyependa kuishi maisha ya ufukara na unyenyekevu. Chumaba chake kilikuwa na kitanda bila godoro, meza iliyojaa karatasi nyingi za kujisomea, kiti na mahali pa kunawia. Kilikuwa ni chumba ambapo aliwasikiliza waamini, na wakati mwingine kiligeuka kuwa ukumbi wa shughuli za shule ya watoto aliyokuwa kaanzisha, alikuwa akila chakula pamoja na wafanyakazi wake, na alikuwa mkarimu wa kupokea kila mtu.

Tarehe 20 Juni 2017, Baba Mtakatifu Francisko atafanya hija ya kitume huko Barbiana ikiwa ni kumbukumbu ya miaka 50 tangu Padre Lorenzo Milani alipofariki dunia. Tukio hili ni la kugusa sana mioyo na kufungua macho kwa wengi kumtazama Padre Lorenzo kama nabii wa mtindo wa maisha uliokuwa unahitajika kugeuzwa nyakati za utume wake, kwani ni katika miaka hiyo ndipo Baba Mtakatifu Yohane XXIII anaitisha Mtaguso wa Pili wa Vatican. Mtaguso uliotoa mafundisho ya umuhimu wa kufungua madirisha na milango kwa ajili ya kukutana na kuwapokea wanadamu wote, kuishi maisha ya kijumuiya zaidi, na ushiriki wa kila mwamini katika maisha na utume wa Kanisa.

Kanisa kwa sasa linaye Baba Mtakatifu Francisko ambaye anawapigania zaidi maskini na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, anawaalika mapadri, watawa wa kike na wa kiume na waamini wote kuwa na wongofu wa ndani, kuepuka tamaa ya mali na madaraka, kuwa wanyenyekevu, wakarimu na kutokomeza aina zote za utengano na matabaka. Mtindo huu wa maisha aliuishi kwa kina Padre Lorenzo Milani, na wengi hawakuweza kumuelewa nyakati zake.

Pamoja na hali ya kutoeleweka na wengi kipindi chake, Padre Lorenzo aliandika katika barua mwaka 1958 kwamba, hatothubutu kujitenga na Kanisa, sababu kwa kila juma alihitaji huruma ya Mungu mara nyingi, na alitambua kuwa anaipata katika Kanisa katoliki peke yake, hivyo kujitenga na Kanisa asingeweza kupata mahali pengine pa kukimbilia huruma hiyo. Kwa sababu hiyo akawa mvumilivu, mtii na mnyenyekevu huku akitenda utume kwa bidii na moyo mkuu mpaka siku mauti ilipomfika mnamo tarehe 26 Juni 1967.

Katika hija yake ya kitume maeneo ya Toscana, Baba Mtakatifu Francisko atapita pia Bozzolo kwa heshima ya kumbukumbu ya Padre Primo Mazzolari, padre ambaye wakati wa maisha yake alihubiri na kuishi Injili inayomwilishwa katika maisha ya kila siku ya mwanadamu kadiri ya changamoto na hali halisi za wakati na mahali. Padre Mazzolari alipadirishwa tarehe 24 Agosti 1912, akapangiwa kuhudumia Spinadesco na baadae akahamishiwa kwenye Seminari ya Cremona kama mwalimu wa somo la Fasihi Andishi. Baadae akawa paroko wa Bozzolo na alifariki tarehe 12 Aprili 1959.

Padre Mazzolari alikuwa anasema kwamba parokia ni kama gari la wagonjwa, ambulance, ambalo lazima liwe tayari kila wakati kuwakimbilia na kuwahudumia wale wanaopata hitilafu ya afya wakati wowote katika hija ya maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko amesikika mara kadhaa akilitambua Kanisa kama Hospitali katika Uwanja wa mapambano. Namna hii ya mtazamo unawaunganisha Padre Mazzolari na Baba Mtakatifu katika kuwajali na kuwahudumia maskini na wanyonge, umwilisho wa Injili ya ukarimu.

Kwa miaka ya nyuma, kumekuwa na mwelekeo wa baadhi ya watu kutia chumvi juu ya mtindo wa maisha ya Padre Primo Mazzolari kana kwamba alikuwa mtu wa kushabikia mambo ya siasa. Hata hivyo ukweli ni kwamba, padre huyu alikuwa mtumishi wa Mungu kati ya watu, na aliguswa na maisha ya kila siku ya waamini, ambayo huwezi ukayatenganisha na maisha yao kiimani, anasema Askofu Antonio Napolioni wa jimbo la Cremona nchini Italia.

Kwa upande wake Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu katoliki Italia anasema, mapadri hawa wawili wanapotazamwa leo kama manabii, wasieleweke sana kana kwamba walikuwa wakihubiri mambo yaliyopaswa kutokea siku za baadae. Nabii wa mungu kwanza kabisa, ni mtu anayesikiliza sauti ya Mungu kiasi cha kuweza kufahamu kiini cha changamoto za maisha, na kuwa na uwezo wa kufanya mang’amuzi kwa kukabiliani nazo kadiri ya ishara za nyakati.

Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 

 

 

17/06/2017 14:17