Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Familia ya Mungu nchini Ujerumani inaomboleza kifo cha Helmut Kohl

Familia ya Mungu nchini Ujerumani inaomboleza kifo cha Helmut Kohl, Baba wa muungano wa Ujerumani. - AP

17/06/2017 17:19

Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani linamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya ushuhuda wa maisha ya Kikristo, uliooneshwa na Chancellor Helmut Kohl wa Ujerumani aliyefariki dunia, Ijumaa tarehe 16 Juni 2017 akiwa na umri wa miaka 87. Ni kiongozi aliyesimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu na uhuru wa kijamii. Ni kiongozi aliyeamini katika umoja na mshikamano, akathubutu kubomoa ukuta wa Berlin uliokuwa unawatenganisha na kuwagawa Wajerumani kwa itikadi zao.

Marehemu Chancellor Helmut Kohl alisimamia uchumi jamii na soko huru kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa! Alikuwa na maono mapana sana na mwamini wa umoja na majadiliano kwa ajili ya mafao ya wengi! Alikuwa ni kiungo muhimu sana katika mchakato wa Mkataba wa Maasstricht, uliopelekea Umoja wa Ulaya kuwa na Sarafu moja inayowaunganisha wote. Hivi ndivyo Kardinali Reinhard Marx anavyoandika katika salam za rambi rambi kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani.

Ni kiongozi aliyejipambanua katika masuala ya uongozi tangu mwaka 1982 hadi mwaka 1998 alipong’atuka kutoka madarakani. Alionesha mshikamano na viongozi wa Kanisa hadi kufanikisha hija za kichungaji za Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Ujerumani katika mwaka 1987 na mwaka 1996, kwa pamoja wakavuka Lango la Brandeburg, kielelezo cha uhuru na uwajibikaji, ili kuondokana na mawazo mgando yanayoweza kuwarejesha tena watu katika tabia na mfumo wa mazoea ya maisha. Alipenda kuonesha upendo kwa Mungu na jirani. Kwake, Injili ya Kristo ilikuwa ni chemchemi ya nguvu, umoja, upendo na mshikamano; tunu msingi zilizosaidia ujenzi wa Jumuiya ya Ulaya. Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani linasikitika sana kwa kifo cha Chancellor Helmut Kohl, wakati huo huo, linamshukuru Mungu kwa zawadi ya kiongozi shupavu kama Kohl aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuiongoza familia ya Mungu nchini Ujerumani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

17/06/2017 17:19