2017-06-16 15:27:00

Rushwa na ufisadi ni chanzo cha majanga na maafa ya binadamu!


Kardinali Peter Turkson amefanikiwa kuchimbua mizizi ya maeneo yanayoweza kuchochea kishawishi cha rushwa na ufisadi. Ameanza katika maisha ya kiroho, yaani kutoka katika undani wa mtu mwenyewe na kupanua wigo huu katika maisha ya kijamii, kisiasa, kitamaduni na kiuchumi sanjari na kuelezea dhamana na wajibu wa Mama Kanisa katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, saratani inayopekenyua maisha ya mataifa mengi duniani, kiasi cha kukwamisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Hii ni changamoto pevu katika maisha, utume na utambulisho wa Kanisa, ndivyo anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji ya kitabu kuhusu “Rushwa” kilichoandikwa na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu baada ya kufanya mahojiano na Bwana Vittorio V. Albert. Kardinali Turkson anasema, Kanisa halina budi kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; uhalifu wa magenge kitaifa na kimataifa. Ili kufanikisha mapambano haya, rushwa haina budi kushughulikiwa kama “chuma chakavu” ndani ya Kanisa kwa kujikita katika: kanuni maadili, utu wema sanjari na kuambata tunu msingi za Kiinjili.

Kwa njia hii, Kanisa litaweza kuongoza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Lakini kwanza kabisa, Kanisa halina budi kuwa safi pasi na mawaa wala makunyanzi ya rushwa na ufisadi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, rushwa ni mchakato unaoharibu na kuvunjilia mbali kabisa mafungamano,upendo na mshikamano wa binadamu. Rushwa inatia doa uhusiano kati ya binadamu, Mwenyezi Mungu na kazi ya uumbaji. Lakini kinyume cha rushwa ni: Uaminifu, uadilifu, utu wema, upole na unyofu wa moyo mambo yanayopania kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Rushwa inaonesha maisha ya mwanadamu asiyekuwa na  dira wala mwelekeo sahihi wa maisha, hali inayoharibu sana mafungamano ya kijamii. Matokeo yake ni kukomaa kwa ubinafsi usiokuwa na mvuto wala mashiko; tabia ya kutowajali wengine. Rushwa inaonesha ile roho ya korosho, roho ya kwa nini; roho ya kutu, roho iliyovunda na kuanza kutoa harufu mbaya. Rushwa ni kikwazo katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rushwa inapelekea kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Ni chanzo kikuu cha kuibuka na kusambaa kwa magenge ya kihalifu, kitaifa na kimataifa; magenge yanayochochea utamaduni wa kifo.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ili kupambana na rushwa pamoja na ufisadi kuna haja ya kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi, kimaadili, kitamaduni na kiutu! Hii inatokana na ukweli kwamba, rushwa inapata chimbuko lake katika moyo wa mwanadamu! Rushwa ina tabia ya kujigeuza geuza kadiri ya mazingira na vionjo vya mtu, kumbe, hakuna anayeweza kujidai kwamba, rushwa ameipatia kisogo! Jambo la msingi ni kuwa macho na makini; kwa kukesha na kusali, ili kutokutumbukia majaribuni!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua katika utangulizi wa kitabu kuhusu “Rushwa” kwamba, ina tabia ya kutaka kutanuka na kujigamba; kusambaa na kuenea kwa haraka kama moto wa mabua! Ina tabia ya kujikweza na kujiona bora kuliko wengine, kiasi cha mtu kuweza kujenga dharau na tabia ya kutowajali wengine! Mdhambi anaweza kuwa na ujasiri wa kuomba msamaha, lakini mla rushwa na fisadi ni watu wenye moyo mgumu na ni vigumu sana kuomba msamaha. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa halina budi kusikiliza kwa makini na kuwa na ujasiri wa kunyanyuka na kuanza kuganga na kuponya madonda na majeraha ya ukosefu wa matumaini mintarafu huruma ya Mungu. Kanisa lifanye kazi hii kwanza kabisa kwa kujisafisha lenyewe, bila woga wala makunyanzi.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, rushwa ndani ya Kanisa ni ile tabia ya wakleri, watawa na waamini kupenda na kumezwa mno na malimwengu; inajionesha katika utepetevu wa imani; tabia ya unafiki na watu kutaka umaarufu wa mpito, tamaa ya mali na madaraka. Kanisa linaweza kushinda kishawishi cha rushwa na ufisadi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kumjengea uwezo wa kutoka kifua mbele ili kulinda na kudumisha mambo msingi. Kanisa halina budi kujielekeza katika kusimamia na kutekeleza misingi ya haki , huruma na upendo; kwa kukazia kipaji cha ubunifu, umoja na mshikamano, ili kupyaisha maisha ya binadamu dhidi ya rushwa na ufisadi, sumu kali dhidi ya utu na heshima ya binadamu!

Rushwa ni mapambano yanayowashirikisha watu wote kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kukazia majiundo makini na endelevu yanayofumbatwa katika utamaduni wa huruma ya Mungu. Ni mapambano yanayohitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa watu wote wenye mapenzi mema, ili kutambua na hatimaye, kutibu na kuganga saratani ya rushwa.

Mwandishi wa Kitabu cha “Rushwa” katika Sura ya Kwanza ya Kitabu anakazia juu ya ufafanuzi unaotolewa na Kardinali Turkson juu ya maana ya rushwa; dhamana na wajibu wa Kanisa katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu; dhana, uwepo, tamaa ya dhambi na madhara yake katika maisha ya mwanadamu. Umuhimu wa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu kama sehemu ya ukuzaji wa mafungamano ya kijamii. Sura ya Pili inajikita katika “Mtu” ambaye anaweza kupoteza uhuru, utu na heshima yake kwa kuendekeza rushwa, inayomgeuza kuwa mtumwa!

Hapa kuna haja ya kukazia toba na wongofu wa ndani kama alivyofanya Zakayo Mtoza Ushuru alipokutana na Kristo Yesu. Rushwa bado inajitokeza katika sura ya kazi, cheo; unafiki na tabia ya kuridhika na mambo ya chini pasi na kufanya juhudi za kuboresha maisha, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi. Watu wakijidekeza kwa kupenda mno anasa, tafrija, mali na uchu wa madaraka, kishawishi cha rushwa kitawabwaga chini, wapende wasipende anasikitika kusema, Kardinali Turkson.

Sura ya tatu inazungumzia “Jamii” inayojikita katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, kiasi cha kubeza kanuni maadili na utu wema; kwa kutaka faida kubwa na kwamba, binadamu na mahitaji yake msingi si mlengwa wa mchakato wa uzalishaji na huduma, bali fedha ndiyo inayotafutwa na kupewa kipaumbele cha kwanza. Rushwa ni saratani ya jamii inayoweza kuponywa kwa familia ya Mungu kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini; kwa kujielekeza katika elimu na huduma bora ya afya! Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, hata “Vatican kuna rushwa” ndiyo maana aliandika “Maradhi 11 ya Sekretarieti Kuu ya Vatican.

Sura ya Nne ni juu ya “Uhalifu”. Kardinali Turkson anasema, rushwa, ufisadi na uhalifu wa magenge ni sawa na “uji kwa mgonjwa”  au ni sawa na “chanda na pete” kamwe havitengamani. Haya ni matunda ya ubinafsi, uchu wa mali na madaraka. Mwaliko wa Kanisa hapa ni toba na wongofu wa ndani; msamaha na upatanisho; Injili ya matumaini kwa kuboresha mfumo wa elimu, ili kweli elimu inayotolewa iwe bora; kwa kukazia utawala wa sheria, haki na demokrasia makini.

Sura ya tano inazungumzia ”Uzuri na wema” kwa kukazia umuhimu wa elimu na majiundo makini ya awali na endelevu; wongofu wa ndani na wa kifikra; umoja, mshikamano na mafungamano ya kijami; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Yote haya hayana budi kusimikwa katika ukweli na uwazi; uadilifu na utu wema; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni dawa mchunguti, kiboko ya tabia ya rushwa na ufisadi! Jaribu kuyatekeleza, utagundua siri ya mafanikio!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.