Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Jubilei ya miaka 200 Kanisa katoliki Afrika kusini

Miaka 200 ya Uinjilishaji kusini mwa Afrika, mwaka wa mshikamano - REUTERS

16/06/2017 14:55

Kanisa katoliki nchini Afrika ya kusini linaelekea kuadhimisha miaka 200 ya uinjilishaji nchini humo, tangu Baba Mtakatifu Pius VII alipounda Vikarieti ya kitume ya Cape of good hope na maeneo yaliyokuwa yakipakana nayo, mnamo tarehe 7 Juni 1818. Kwa sasa Kanisa kusini mwa Afrika ina majimbo 28 na Vikarieti ya kitume moja katika Shirikisho la Baraza la Maaskofu kusini mwa Afrika (SACBC), ambalo linajumuisha nchi za Afrika ya kusini, Botswana na Swaziland.

Maadhimisho hayo ya Jubilei ya miaka 200 ya Uinjilishaji Afrika ya kusini yatazinduliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu kumshukuru Mungu, itakayofanyika kwenye Kanisa kuu la Our lady of the Flight into Egypt, Jimbo kuu la Cape town, siku ya Jumapili tarehe 25 Juni 2017, majira ya saa 9 alasiri kwa saa za Afrika ya kusini. Kati ya waalikwa ni pamoja na Maaskofu kutoka Botswana na Swaziland, Australia na visiwa vya Mauritius ambao walikuwa sehemu ya Vikarieti ya Cape of good hope iliyoundwa mwaka 1818 na Baba Mtakatifu Pius VII. Maaskofu kutoka nchi hizo, wanakaribishwa pia kuendelea kufanya hija nchini Afrika kusini kwa muda wote wa maadhimisho ikiwa ni sehemu ya kuonesha mshikamano na kanisa ambalo kwao ni chimbuko la imani.

Katika adhimisho hilo la uzinduzi, watakumbukwa kwa heshima wanaume na wanawake waliojitoa kwa ujasiri katika historia hiyo ya miaka 200 kwa ajili ya uinjilishaji na ukuaji wa Kanisa nchini humo. Hawa ni pamoja na mapadri, watawa wa kike na wa kiume na waamini walei. Pia katika kuadhimisha sikukuu ya Watakatifu Wote, ambapo Kanisa Jimboni Cape town litaadhimisha Jumapili ya tarehe 5 Novemba 2017, itafanyika kidekania kwa ajili ya kuwakumbuka watumishi mbalimbali waliolihudumia jimbo hilo na sasa wamekwishatangulia mbele ya Kiti cha Haki cha Mwenyezi Mungu.

Katika sherehe za uzinduzi, kila Askofu Jimbo wa Afrika kusini, Botswana na Swaziland atakabidhiwa mshumaa unaowaka uliopambwa vizuri kuashiria ushamiri na ushuhuda yakinifu wa imani kwa miaka hiyo 200. Mshumaa huo utawekwa katika Kanisa kuu la kila jimbo na kuwashwa katika maadhimisho matakatifu wakati wa mwaka huo wa Jubilei (Juni 2017 – Juni 2018). Mapdri watapewa pia nakala ya Waraka wa Tamko la kuundwa Vikarieti ya Cape of good hope iliyotolewa na Baba Mtakatifu Pius VII, mnamo 1818. Nakala hiyo itapaswa iwekwe mahali fulani pa wazi katika kila Parokia kusini mwa Afrika. Zaidi kutakuwa na maandamano ya Ekaristi Takatifu Jimboni Cape town, kutoka Parokia ya Msalaba Mtakatifu, District six, kuelekea kwenye ngazi za Kanisa kuu la Jimbo hilo, ambapo waamini watapokea Baraka kuu. Wakati wa maandamano ya Ekaristi Takatifu kutakuwa na sala kwa ajili ya kuombea familia, vijana, wazee, wagonjwa, wakimbizi na wahamiaji.

Wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 ya uinjilishaji, Jimbo kuu la Cape town linasisitiza sana utume wa pamoja, mshikamano na udugu ili kuboresha huduma za kichungaji. Kwa sababu hiyo mapadri viongozi wa dekania wanahimizwa sana kuhamasisha umoja na mshikamano huo katika dekania zao. Katika hilo, Askofu mkuu Stephen Brislin wa Cape town, ameazimia kwamba wakati wa maadhimisho ya Jubilei, Sakramenti ya Kipaimara, badala ya kuadhimishwa kiparokia, itaadhimishwa kidekania.   

Padre Clifford Stokes, Makamu wa Askofu Jimbo kuu la Cape town, kwa niaba ya Kanisa Jimboni humo, anatoa shukrani za dhati kwa Mashirika ya kitawa kwa huduma nzuri ambayo wamekuwa wakiitoa katika sekta za elimu, afya na kuwajali maskini. Katika kuboresha malezi bora ya vijana hasa mashuleni, shule zinazoendeshwa na Kanisa jimboni Cape town, zitakuwa na utaratibu wa kutoa nafasi kwa wanafuzni kushirikisha historia za maisha yao hasa manufaa na changamoto katika majiundo yao kwenye shule za Kanisa. Masimulizi hayo ya wanafunzi yatachapishwa katika Jarida la kijimbo na kusambazwa ili watu wengi zaidi waweze kushiriki ushuhuda huo.

Kilele cha maadhimisho ya Jubilei hiyo kitaadhimishwa Jumapili ya terehe 10 Juni 2018, katika kila Kanisa kuu la kila jimbo kusini mwa Afrika, ambapo ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa ajili ya Jubilei hiyo utasikika hewani, ule mshumaa utakaokuwa umegawiwa wakati wa uzinduzi utakuwa ukiwaka na kung’ara, kengele za Makanisa hayo makuu zitapigwa, bila kusahau shangwe, ndelemo na vigelegele kuashiria umoja na mshikamano katika furaha ya Injili, Evangelii gaudium.

Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

16/06/2017 14:55