2017-06-16 16:50:00

Askofu Jean Benoit Bala aliuwawa kikatili nchini Cameroon!


Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon, limehitimisha mkutano wake usiokuwa wa kawaida na kutoa tamko kwamba, Askofu Jean Benoit Bala wa Jimbo Katoliki Bafia, aliuwawa kikatili na wala hakujinyonga kama ilivyodaiwa hapo awali. Kanisa Katoliki nchini Cameroon linapitia kipindi kigumu katika historia, maisha na utume wake, baada ya Askofu Bala kupotea katika mazingira ya kutatanisha na hatimaye, kukutwa ametumbukizwa mtoni baada ya kuuwawa kikatili.

Askofu Jean Benoit Bala alikutwa amefariki dunia kwa kutumbukizwa mtoni tarehe 2 Juni 2017, mwili wake ukaokotwa na mvuvi, umbali kidogo kutoka katika Daraja la “Childhood”. Askofu Mkuu Piero Pioppo, Balozi wa Vatican nchini Cameroon, Askofu Samuel Kleda, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon pamoja na Askofu mkuu Jean Mbarga wa Jimbo kuu la Yaounde pamoja na viongozi wa kidini na serikali. Hadi wakati huu, mwili wa marehemu Askofu Jean Benoit Bala wa Jimbo Katoliki Bafia bado umeshikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya uchunguzi, ili kubaini kile kilichosababisha kifo cha Askofu Balla, ili hatimaye, sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Familia ya Mungu nchini Cameroon imeshtushwa sana na kutokana na mauaji haya. Haya ni mauaji ya kikatili yanayoendelea kutokea nchini Cameroon kama ilivyotokea kwa Askofu Yves Plumey, mwaka 1991,  Askofu Abbè Joseph Mbassi mwaka 1988, Padre antony Fontegh mwaka 1990, Watawa wa Djoum pamoja na Padre Engelbert Mveng. Hawa ni baadhi ya viongozi wa Kanisa ambao damu yao ni ushuhuda wa nyanyaso na dhuluma dhidi ya Kanisa nchini Cameroon.

Kutokana na mazingira tatanishi ya kifo cha Askofu Askofu Jean Benoit Bala, Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon inataka ukweli wote kuhusu mauaji ya Askofu huyu: Wahusika wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake. Serikali inapaswa kusimama kidete kulinda na kudumisha ulinzi na usalama wa maisha ya raia na mali zao. Maaskofu wanasubiri kwa hamu kusikia hatima ya uchunguzi wa Serikali. Maaskofu wanavitaka vyombo vya mawasiliano ya jamii kuheshimu Injili ya uhai; kulinda, kutetea na kudumisha: utu wa binadamu, ukweli, weledi, kanuni na maadili ya kazi.

Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon linaitakia familia ya Mungu nchini humo amani na utulivu; ujasiri na uvumilivu kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu, ameushinda ulimwengu. Viongozi wao wa Kanisa wako pamoja katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Wanawataka waamini kujichotea nguvu kutoka katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Waendelee kusali na kuwaombea viongozi wa Kanisa waliofariki dunia katika mazingira ya kutatanisha bila kusahau kuombea: haki na amani nchini mwao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.