Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Ushuhuda wa imani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu!

Ekaristi Takatifu ni muhtasari wa imani ya Kanisa, ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. - L'Osservatore Romano

15/06/2017 09:08

Askofu Mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya katika mahojiano maalum na Radio Vatican anafafanua: maana na umuhimu wa maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu ambayo kimsingi ni sadaka ya Fumbo la Pasaka linaloadhimishwa na Mama Kanisa kila siku! Maandamano ya Ekariti Takatifu ni ushuhuda wa imani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu linalodhihirisha uwamo wa Yesu katika Maumbo ya Mkate na Divai. Ekaristi Takatifu ni muhtasari wa imani ya Kanisa, ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Ekaristi Takatifu ni alama ya shukrani kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu katika kazi ya uumbaji, ukombozi na utakatifushaji. Ekaristi Takatifu iliwekwa rasmi na Yesu, Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, akaamua kuwapatia wafuasi wake Mwili na Damu yake, ili uweze kuwa ni chakula cha maisha yao ya kiroho, tayari pia kujisadaka kwa ajili ya jirani zao katika mchakato mzima wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu! Kwa ufupi, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Sadaka, shukrani, kumbu kumbu na uwepo endelevu wa Kristo miongoni mwa wafuasi wake.

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde anasema, maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu yanafanywa kwa kishindo kikuu kama ilivyokuwa Siku ile Yesu alipoingia Yerusalemu, akashangiliwa na watoto wa Wayahudi waliokuwa wamebeba matawi ya mizeituni huku wa kiimba kwa furaha ”Hosana juu mbinguni, mbarikiwa anayekuja kwa jina la Bwana”. Wakati wa Sherehe ya Ekaristi Takatifu, waamini wanamtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu Mfalme wa: upendo, haki na amani, ukweli na uzima; Utakatifu, neema na baraka. Kanisa linakiri uwamo wa Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai. Huyu ndiye Yesu anayeambatana na waja wake katika hija ya maisha yao ya kila siku!

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde anasema, Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani, kwani kwa macho ya kibinadamu watu wanaona maumbo ya Mkate na Divai, lakini kwa imani waamini wanakiri uwepo wa Yesu katika Sakramenti ya ajabu, kilelezo cha upendo wake usiokuwa na kipeo. Kanisa na ulimwengu wanalo hitaji kubwa la Ibada ya Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Upendo. Mtakatifu Thoma wa Akwino anakaza kusema uwepo wa Mwili kweli wa Kristo, na wa Damu kweli ya Kristo katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, hauwezi kufahamika kwa milango ya maarifa, bali kwa njia ya imani peke yake. Hii ndiyo Karamu ya Pasaka, amana na utukufu wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

15/06/2017 09:08