2017-06-15 14:09:00

Ushirikiano wa Afrika na Ulaya kuhudumia wahamiaji wakomaza matunda


Taarifa iliyowasilishwa tarehe 13 Juni 2017 na Bi Federica Mogherini, Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jumuiya ya Ulaya, inaonesha matumaini makubwa katika kukabiliana na changamoto ya wahamiaji kutoka Barani Afrika. Mwaka sasa umetimia tangu kuwe na makubaliano ya pamoja ya ushirikiano kuhusu wahamiaji, makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Umoja wa Ulaya na nchi tano za Afrika, Niger, Mali, Nigeria, Senegal na Ethiopia. Lengo ni kukabiliana vema na changamoto ya wahamiaji, na kutokomeza biashara haramu ya binadamu.

Taarifa iliyotolewa hivi karibuni katika Kamati ya Umoja wa Ulaya kuhusiana na ushirikiano huo, imeweka wazi kwamba kumekuwa na mafanikio makubwa ambapo wahamiaji wengi wa nchi hizo tano za Afrika, ambao walikuwa wamekwama njiani kuelekea Barani Ulaya, wameshawishiwa na kuridhia kurudi nchini mwao, kwa hiari bila shuruti, tena kwa moyo radhi.

Kati ya mafanikio ni pamoja na kujegwa kwa ofisi zinazoshughulikia wahamiaji za Umoja wa Ulaya katika nchi hizo tano za Afrika. Ofisi hizo zinahusika na miradi mbali mbali ili kutengeneza fursa za kazi, kuboresha uwezekano wa kupata elimu na mafunzo mbali mbali na pia kusaidia uangalizi wa mipaka katika nchi za Niger, Mali, Nigeria, Senegal na Ethiopia. Nchi hizi ni kati ya nchi za Afrika zinazoongoza kwa kuwa na wakimbizi na wahamiaji wengi Barani Ulaya. Katika taarifa yake hiyo, Bi Federica Mogherini anahitimisha kwa kusema kwamba, ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na nchi hizo tano za Afrika kumeleta mafanikio makubwa sana yanayoonekana wazi katika kukabiliana na changamoto ya wahamiaji na biashara haramu ya binadamu.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.