2017-06-15 14:34:00

Taratibu mpya za kesi za ndoa, nyenzo kuboresha maisha ya waamini


Ni takriban mwaka na nusu sasa tangu Baba Mtakatifu Francisko alipoweka mabadiliko katika taratibu za uendeshaji wa kesi za ndoa katika mahakama za Kanisa. Ilikuwa mwezi Agosti 2015, ambapo Baba Mtakatifu Francisko kwa Barua binafsi, Motu proprio, Mitis Iudex Dominus Iesus, yaani Yesu Kristo Bwana Hakimu mwenye Haki, alifanya mabadiliko hayo kwa nia ya kufupisha mchakato wa uendeshaji wa kesi za ndoa, ili kuepuka kesi hizo kuwa ndefu sana, kutumia gharama nyingi na waamini kubaki muda mrefu bila kufahamu hatima ya kesi zao.

Mahali pengi taratibu hizi zimekuwa zikitafsiriwa visivyo na kuwafanya baadhi ya watu kuamini kwamba talaka zimeruhusiwa katika Kanisa Katoliki. Mambo si hivyo! ndoa ya kikatoliki inabaki kuwa ndoa halali iwapo ilifungwa kwa kufuata taratibu za Kanisa, na mchakato wa kutangaza ndoa hizo batili, iwapo zilikuwa hivyo tangu awali, unaendelea kufuata kanuni za vizuizi zilizopo kwenye Kanuni sheria za Kanisa. Hivi karibuni nchini Italia, Majarimu wawili wa sheria za Kanisa katika Chuo kikuu cha Lateran, Prof. Manuel Jesus Arroba Conde na Prof. Claudia Izzi, wametoa kitabu (Pastorale giudiziaria e prassi processuale nelle cause di nullità del matrimonio. Dopo la riforma operata con il Motu proprio Mitis Iudex Dominus Iesus), kuhusu sheria za kichungaji na taratibu za kesi za ndoa kufuatia Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu mabadiliko ya taratibu za kesi za ndoa kanisani, Mitis Iudex Dominus Iesus, yaani Yesu Kristo Bwana Hakimu mwenye Haki.

Kitabu hicho kinaelezea kanuni zinazozingatiwa katika ufunguzi, uendeshaji na maamuzi ya kesi za ndoa kwenye mahakama za Kanisa. Ni nyenzo kwa waamini kufahamu namna ya kujiandaa kuomba kufungua kesi ya ndoa, vitu vya msingi vya kuzingatia, kujieleza kwa kila mwana ndoa mhusika, uwasilishi wa ushahidi wa nyaraka na wa mashahidi mbali mbali. Katika mfumo mpya wa kesi za ndoa, ule utaratibu wa kupeleka hukumu kwenye mahakama ya rufaa ili ithibitishwe, kwa sasa umefutwa. Kwa sasa kesi ikishaamuliwa na mahakimu wa mahakama ya awali, hukumu hiyo inafanyiwa kazi, isipokuwa tu kama mmoja wa wahusika atakata rufaa, ndipo itapelekwa mahakama ya rufaa kadiri ya taratibu.

Kama tulivyotangulia kusema awali, Sakramenti ya ndoa inabaki na hadhi yake, na sio kushabikia talaka, bali kujisadaka kwa wana ndoa ili kumshuhudia Kristo kwa kuishi utakatifu katika maisha ya ndoa. Magumu katika maisha ya ndoa yapo siku zote, suluhu sio kukimbia, kuhama au kubadili. Ni muhimu kuwa kweli msaidizi kwa mwenza wako (Rej. Mwanzo 2:18), ili kwa pamoja wana ndoa muweze kuirithi mbingu. Pamoja na fadhila ya uvumilivu na kusaidiana kwa wana ndoa, ni muhimu pia kuwa wakarimu, yaani kutokuwa mwiba ndani ya familia. Kila mmoja ajitahidi kuwa mwaminifu hata inapobidi kujisadaka kikubwa, kila mmoja ajali hisia za mwenzie, na kuepuka makwazo kila siku yasiyo na tija.

Kwa sababu hizo, pamoja na taratibu mpya za kuendesha kesi za ndoa, kabla ya kufikia hatua ya kupeleka kesi katika mahakama za ndoa, ni muhimu kutafuta suluhu na kuboresha maisha ya ndoa na familia. Hapa wanaalikwa watu wengine wa karibu kushiriki katika kuwasaidia wana ndoa. Wanaalikwa wana familia, wachungaji mapadri, waandaaji wana ndoa mfano makatekista na watu wa taaluma mbali mbali wanaoshirki katika maaandalizi ya ndoa (Amoris laetitia Na. 244). Lengo liwe ni kudumisha na kuthamini maisha ya ndoa na familia, ili kulishudia pendo la Kristo kwa wafuasi wake, pendo na uaminifu wa Kristo kwa Kanisa lake.

Ieleweke kwamba sheria kanuni za Kanisa hazina lengo la kuumiza waamini, wala sio nyenzo ya kubeza mafundisho ya Kanisa kwa kuruhusu talaka, bali ni nyenzo ya kurahisisha maisha ya waamini kwa kuzingatia ukweli wa mafundisho ya Kanisa na mapenzi ya Mungu. Uasilia wa Kanisa ni maisha ya umisionari, utangazaji wa Injili kwa ajili ya wokovu wa watu: Hivyo hata sheria kanuni za Kanisa zina lengo hilo hilo la wokovu wa roho za watu. Hilo linajidhihirisha katika sheria kanuni Nambari 1722 inayoweka wazi kwamba: katika taratibu zote za sheria kanuni za Kanisa, kipaumbele kipewe kwenye wokovu wa roho za watu.

Ili kujali wokovu wa kila mtu, kuna kanuni msingi ambazo sheria za Kanisa zinazingatia katika taratibu zake. Ni muhimu kuzingatia heshima katika taratibu za sheria, ili haki iweze kutendeka kwa wote, kwani hakuna ukarimu, wala huruma isiyojali haki za wengine. Mungu Mwenyezi ni Mungu wa huruma na haki, anayejali wanyonge na anayedai heshima na utii wa maagizo anayotoa kwa viumbe vyake.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.