2017-06-15 08:10:00

Siku kuu ya Ekaristi Takatifu na Kongamano la Jimbo kuu la Roma!


Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza katika historia, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, Jumapili tarehe 18 Juni 2017, majira ya saa 1:00 kwa Saa za Ulaya ili kuwawezesha waamini wengi zaidi kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu na baadaye maandamano ya Ekaristi Takatifu kutoka katika Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kuelekea kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma. Kadiri ya Mapokeo ya Kanisa, Sherehe hii ilikuwa inaadhimishwa mjini Vatican Alhamisi, iliyokuwa inafuatia baada ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kardinali Agostino Vallini, Makamu wa Askofu mstaafu, katika barua yake kwa Mapadre wa Jimbo kuu la Roma, anawaalika Maparoko kuandamana na waamini wao ili kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu, maarufu kama “Corpus Domini”. Ni wakati muafaka wa kuimarisha ushuhuda wa waamini katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu hadharani, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo katika maisha ya waamini wake. Kuanzia sasa maadhimisho haya yatakuwa yanafanyika Jumapili badala ya Alhamisi kama ilivyozoeleka kadiri ya Mapokeo, ili kuweza kuunganika na Makanisa mengine mahalia kumwabudu na kumshuhudia Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Parokia za Jimbo kuu la Roma zimepewa fursa ya kuweza kuadhimisha Sherehe hii kwa mkesha Parokiani kwao, ili hatimaye, Jumapili, wote kwa pamoja waweze kuonesha mshikamano na ushuhuda wao pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Kardinali Agostino Vallini katika barua yake kwa Maparoko aligusia pia kuhusu Kongamano la Jimbo kuu la Roma, litakalozinduliwa Jumatatu, tarehe 19 Juni 2017, majira ya saa 1:00 kwa saa za Ulaya, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano. Kongamano la mwaka huu linaongozwa na kauli mbiu “Majiundo makini kwa vijana wanaopevuka”. Tema hii ni matunda ya tafakari ya kina inayotaka kuimarisha furaha ya upendo ndani ya familia, ili kweli familia za Kikristo ziweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu!

Kwa namna ya pekee, Kongamano la Jimbo kuu la Roma linataka kuimarisha dhamana na wajibu wa wazazi na walezi kwa watoto wao katika masuala ya maadili na utu wema. Kongamano litazinduliwa kwa tafakari elekezi itakayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, kongamano linatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 18 Septemba 2017 kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano: Asubuhi, Wakleri wote wa Roma watakutana kwa tafakari ya kina na hatimaye jioni waamini walei wanaojihusisha kwa karibu zaidi katika shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Roma watahudhuria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.